Mwandishi Wetu, Dubai.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro amefanya mazungumzo na Uongozi wa juu wa Shirika la ndege la Umoja wa Falme za Kiarabu la Emirates kwa lengo la kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania ambapo vivutio hivyo vya utalii vitaweza kutazamwa na abiria wapatao milioni 90.2 ambao husafiri kila mwaka kwa kutumia ndege hizo
Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema tangazo hilo litakuwa likitazamwa na mamilioni ya abiria hao kila wakati ndege za Shirika hilo zitakapokuwa zikiruka (take off).
Dkt. Ndumbaro amebainisha hayo leo katika Mji wa Dubai alipokutana na viongozi wa Shirika hilo ambalo mbali ya kusafirisha abiria milioni 90.2 duniani kote pia husafirisha abiria wapatao milioni 20 ambao huunganisha ndege nyingine
Katika hatua nyingine, Dkt. Ndumbaro amesema katika mazungumzo hayo wamekubaliana kutaandaliwa makala tano (Documentaries) za kuelezea vivutio vya utalii vya Tanzania ikiwemo Zanzibar, Serengeti, Ngorongoro pamoja na Mlima Kilimanjaro
''Shirila la ndege la Emirates ni Shirika kubwa sana Duniani lengo letu kama nchi ni kuhakikisha abiria wapatao milioni 90.2 wanaviangalia vivutio vyetu kisha wanavipenda halafu wanatembelea Tanzania'', amesisitiza Dkt. Ndumbaro
Katika mazungumzo hayo, amesema uongozi wa ndege hizo umeonesha utayari wa kushirikiana katika kuitangaza Tanzania kiutalii na ikifika mwanzoni mwa mwezi wa tano mwaka huu wataingia makubaliano (MOU) baina ya Tanzania na Shirika hilo.
Akifafanua mazungumzo hayo, Dkt. Ndumbaro amesema kati ya abiria watakaoangalia vivutio wengi wao watavutiwa na hatimaye sehemu ya watu hao waweze kuja kutembelea Tanzania.
"Shabaha yetu kubwa kama nchi ni kuhakikisha tunafikia watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025, tunaamini tutalifikia lengo hilo", amesisitiza Dkt.Ndumbaro.
Ameongeza kuwa Tanzania inategemea utalii wake wa Wanyamapori kwa asilimia 100 hivyo kupitia mkakati wa kutangaza vivutio vingine vya utalii kama vile utalii wa fukwe, utalii wa utamaduni pamoja na utalii wa ikolojia utaweza kujulikana dunia kote na kuwa chachu ya watalii wengi kuanza kumiminika nchini Tanzania.