Na Mwandishi Wetu
Agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli la kununua korosho yote ya wakulima kwa shilingi 3,300 imeleta kiwewe kwa Kangomba wanaowakopesha fedha au mahitaji ya maisha kwa malipo ya kilo za korosho.
Rais Magufuli amesema “Tutanunua wenyewe korosho yote ya wakulima ili kuhakikisha tunamnufaisha mkulima maskini kwa bei ya shilingi 3,300”
Tafsiri hiyo imewafanya Kangomba kufurahia kwa kuwa wamehakikisha wameyapitia madeni yao yote kwa wakulima kwa madhumuni ya kufaidika na fedha alizozitoa Rais Magufuli kwa mkupuo. Vita hii iliyofanikiwa Wilaya ya Tunduru imewaduwaza na kubaki wasijue la kufanya.
Akiongea na Operesheni korosho Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Juma Zuberi Homera amesema “Wilaya yetu mpaka sasa imekusanya korosho kilo milioni 1,668,910 na idadi ya wakulima waliouza na kulipwa ni 534” ambao wanatoka katika Vyama vya Msingi vya Mtetesi na Chamana.
Mkuu wa Wilaya ameongeza kwa kusema kuwa vita ya kangomba tuliianza mapema mwezi wa Oktoba 2018. Vita hii ni kubwa, pia ngumu sana inahitaji kujituma kwa hali ya juu.
Homera amesema watu walio wengi wanaoshiriki Kangomba ni watumishi wanaohusika na zao la korosho mpaka vyama vya msingi na vile vikuu, ambapo wana mbinu mbalimbali za kuwaibia wakulima ukiacha wale wanaowakopesha wakulima mfano katika kijiji cha Mnenje wakulima walikopeshwa kilo moja ya nyama ya ng’ombe kwa kulipa kilo tano za korosho.
Aidha, Ubabaishaji huo wa kuchukua korosho za wakulima upo zaidi wakati wa kupima kilo za korosho. Yale mawe yanayotumiwa kupima kuna mengine yamethibitishwa na Wakala wa Vipimo Tanzania na mengine ni feki kwa ajili ya kuiba kilo za korosho.
Katika matumizi ya mawe ya kupimia uzito katika vyama vya ushirika ambapo mtu anaweza kupeleka kilo 100 za korosho na Katibu wa cham,a cha AMCOS anayehusika na kupima akamwambia zipo kilo 85 akiwa na maana amemkata kilo 15 ambazo atakuja kujiandikia yeye. Kama kwa siku anawakulima 100 basi kilo hizo zidisha kwa shilingi 3,300 anafaidika sana na fedha za wakulima.
Kutokana na masuala kama hayo wilaya yetu ilikuwa na mtandao mzuri wa kutoa taarifa kila mahali palipo na korosho. Hii imesaidia sana kwa hatua tulizochukua za kukamata korosho za Kangomba na kutaifisha, pia kuwaweka ndani wahusika na kufunguliwa mashitaka.
Kwa wakulima wote 534 waliolipwa hakuna kangomba hata mmoja tulifanya kwa umakini wa hali ya juu kwa kuwa kila tulipopata taarifa ya mtu mwenye korosho ambaye sio mkulima tulifatilia na kudadisi ameipata wapi kwa kiasi kikubwa tumefanikiwa.
Hatua nyingine nilizochukua msimu wa korosho wa mwaka 2017 ni kuvunja Bodi 12 wa vyama vya msingi na watu 56 waliwekwa ndani na kushitakiwa.
Mwisho kabisa nampongeza sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanmzania kwa kumaliza utata wa bei ya korosho lakini naomba tusiharibu dhamira ya Rais kuwa anayetakiwa kulipwa ni mkulima na sio vinginevyo.
Naomba Wtanzania tuwe wazalendo wa kutumikia Umma wa Tanzania kwa moyo wetu wote vinginevyo miaka nenda miaka rudi wakulima watabakia kuwa masikini.