Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Viongozi wa Serikali Watoa Pole Msiba wa Lowassa
Feb 13, 2024
Viongozi wa Serikali Watoa Pole Msiba wa Lowassa
Baadhi ya viongozi Wakuu wakiwa kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo hafla ya kuaga mwili wa Hayati Lowassa imefanyika.
Na Na Ahmed Sagaff - Maelezo

Viongozi wa serikali  wametoa pole kwa Watanzania wote kufuatia kifo cha Mhe. Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu (2005-2008) wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichotokea Februari 10, 2024 katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.

Salamu hizo za pole zimetolewa leo kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ambapo hafla ya kuaga mwili wa Hayati Lowassa ilifanyika huku Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango akiwa mgeni rasmi anayemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan na serikali yote kwa ujumla, ninatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na Watanzania wote kwa msiba huu mkubwa uliotupata," ameeleza Dkt. Mpango.

Naye, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ametoa salamu za pole akisema: "Kwa niaba ya wananchi wote wa Zanzibar, nachukua fursa hii kutoa salamu za pole kwa wanafamilua, ndugu, jamaa na wanafamilia wote kutokana na msiba huu mkubwa kwa mpendwa wetu."

Pamoja na hao, viongozi wastaafu nao wameeleza majonzi yao kufuatia kifo cha Hayati Lowassa.

"Shukrani kubwa ninayoweza kuitoa kwake ni kumuombea kwa Mwenyezi Mungu," ameeleza Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Naye, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein amesema: "Ndugu wananchi! tumeondokewa na kiongozi mwenzetu, na kuondoka huku kila mmoja wetu kutamkuta kwa njia tofauti, wakati tofauti, na siku tofauti. Vitabu vya dini vinatuambia kwamba kila nafsi itaonja umauti."

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Familia ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Monduli, Mhe. Fredrick Lowassa amewashukuru viongozi wa serikali kwa kuifariji familia ya Hayati Edward Lowassa katika kipindi hiki kigumu.

Mwili wa Hayati Edward Lowassa unatarajiwa kuzikwa huko Monduli mkoani Arusha ifikapo tarehe Februari 17, 2024.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi