Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Viongozi wa Dini Waombwa Kutoa Elimu ya Utunzaji Mazingira
Apr 10, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent - RS Tabora

SERIKALI ya Mkoa wa Shinyanga na Tabora imetoa wito kwa viongozi wa dini mbalimbali kuhakikisha wanasaidia katika utoaji wa elimu kwa waumini wao juu ya umuhimu wa upandaji miti na uhifadhi wa mazingira ili kuinusuru mikoa hiyo isijekugeuka kuwa sehemu ya jangwa kutokana na ukataji ovyo wa misitu.

Wito huo umetolewa  mkoani Tabora na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack na mwenyeji wake Aggrey Mwanri wakati wa kongamano la siku moja la mazingira ambalo lilienda sanjari na uzinduzi wa kitalu cha miche na miti 20,000 kwenye ofisi ya Mkoa.

Telack alisema ni vema viongozi wa dini zote kuungana kwa pamoja kuhakikisha wanatumia sehemu ya muda wa kila ibada kuwasisitiza waumini kujenga tabia ya kuhifadhi mazingira, kupanda miti na kuitunza kwa ajili ya manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

“Tunawaomba viongozi wetu wa dini zetu zote kutumia nguvu yenu katika kuwaelimisha waumini wenu juu ya hatari itakayotokea kama tusipotunza mazingira na kupanda miti mipya, tutumie lugha ambayo itasaidia kufikisha ujumbe ili hatimaye nao washiriki kikamilifu katika upandaji miti kwa ajili ya faida ya mikoa yetu na Tanzania kwa ujumla” alisisitiza Mkuu huyo wa Shinyanga.

Alisema pamoja na viongozi wa dini kutoa elimu pia nguvu za pamoja zinahitajika kutoka kwa viongozi, watendaji na wananchi walioko katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na Magharibi na Kati ili kupambana na uharibifu unaofanyika ndani ya misitu ya hifadhi na maeneo mengine na baadhi ya watu kwa maslahi yao.

Telack alisema wapo baadhi ya watu ambao baada ya kuharibu katika maeneo yao wanahamia maeneo mengine ili kuendeleza uharibifu katika misitu ya hifadhi kwa kuanzisha kilimo au kuendesha ufugaji usio rafiki na mazingira na ndio maana ipo haja ya kuunganisha nguvu katika kukabiliana na tatizo hilo.

Vile vile Mkuu huyo wa mkoa wa Shinyanga aliwaagiza Maafisa Uhamiaji kuwachunguza kwa makini baadhi ya watu waliomo katika misitu wakiendesha uharibifu katika misitu ya mikoa hiyo.

“Niliwahi kupitia njia hii katika Wilaya ya Kaliua, nikasimama kununua mahindi kwenye msitu, lakini aliyekuwa akiniuzia alikuwa akiongea Kiswahili ambacho kinaonyesha sio Mtanzania, Uhamiaji fanyieni uchunguzi hilo kuna wageni wako msituni wanamaliza miti yetu” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Alisema baadhi ya watu wanapoulizwa mara nyingi wamekuwa wakisingizia kuwa wanatoka mkoa wa Kigoma lakini ongea yao inaonyesha sio raia wa Tanzania.

Kwa upande wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri alisema wameamua kuanzisha kitalu hicho cha miche 20,000 kwenye ofisi yake ili iwe sehemu ya shamba darasa kwa ajili ya wananchi na wadau mbalimbali kwenda kijifunza juu ya maandalizi ya miche ya miti kwa ajili ya kwenda kuipanda sehemu mbalimbali.

Alisema miche hiyo itagawanywa kwa wananachi mbalimbali kwa ajili ya kuipanda katika maeneo yao kwa utaratibu wa kuwaorodhesha wale wote ambao watakuwa wamepatiwa.

Mwanri aliongeza utaratibu huo wa kuwa na vitalu utashuka hadi ngazi za chini ambapo kila ofisi ya Mkuu wa Wilaya lazima kuwepo na kitalu cha miche 10,000, Afisa Tarafa miche 5,000, Mtendaji Kata miche 2,500 na  Mtendaji wa Kijiji miche 1,250.

Aidha alisema ili kudhibiti uharibifu Serikali itaendelea kusimamia sheria kwa ajili ya kuhakikisha hakuna uharibifu unaofanyika ndani ya misitu ya hifadhi.

Kongamano hilo ambalo lina kauli mbiu ya Tabora na Shinyanga ya kijani inawezekana kila mtu atimize wajibu wake lilitanguliwa na maandamano ya amani kutoka kwenye mnara wa Mwalimu Nyerere hadi ofisi ya Mkuu wa Mkoa

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi