Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Vijiji Vyote Visivyo na Umeme Kupata Umeme Ifikapo 2020/21.
Nov 08, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.

Serikali imesema itahakikisha vijiji vyote visivyo na umeme vinapata umeme kupitia mradi wa kupeleka umeme vijijini awamu ya Tatu (REA-III) unaotegemewa kukamilika mwaka 2020/21.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni, Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Subira Mgalu alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nachingwea Hassan Masala juu ya mpango wa Serikali katika kusambaza umeme katika kata zilizobaki wilayani Nachingwea kupitia REA III.

“Mradi wa REA III utajumuisha vipengele vitatu vya Densification, Grid Extension na Off grid renewable ambapo Mkoa wa Lindi chini ya miradi ya uendelezaji wa grid (Grid extension) katika Mzunguko wa kwanza unatekelezwa kwa muda wa miezi 24 na Kampuni ya Stategrig & Technical Works Ltd,” alifafanua Naibu Waziri huyo.

Aliendelea kwa kusema, katika wilaya ya Nachingwea mpango wa Awamu ya Tatu utavipatia umeme vijiji 30 ambapo kazi za utekelezaji wa mradi zilianza Julai mwaka huu na zinatarajiwa kukamilika Juni 30, 2019.

Mgalu amesema, vijiji vilivyobakia vitapatiwa umeme katika mzunguko wa pili wa REA III utakaoanza Aprili, 2019 hadi Desemba 2021.

Vile vile amesema, kazi ya kupeleka umeme mzunguko wa kwanza itahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 380, ufungaji wa transfoma 18, ujenzi wa njia za msongo wa kilovoti 0.4 zenye urefu wa kilomita  360 na uunganishaji wa wateja 5,710 katika Mkoa mzima wa Lindi.

Aidha amesema, kwa upande wa Wilaya ya Nachingwea jumla ya wateja 1,200 wataunganishwa, ambapo kwa sasa Mkandarasi anaendelea na upimaji wa njia za umeme na tayari amefikia asilimia 30 na kazi za upimaji zitakamilika mwishoni mwa Novemba 2017.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi