Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Vijana, Wanafunzi na Hatari ya Kufanyiwa Uhalifu Mtandaoni
Oct 13, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dar es Salaam

Vijana na wanafunzi ni kundi lenye hatari kubwa ya kukumbwa na uhalifu wa mtandaoni kwa sababu ndio kundi lenye matumizi makubwa ya mtandao kwa ajili ya kufanya utafiti wa masomo, kununua vitu mtandaoni pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii kama twitter, whatsapp, intagram, tiktok n.k.

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika kuadhimisha mwezi wa kujenga uelewa kuhusu usalama mtandao unaoadhimishwa mwezi Oktoba kila mwaka duniani pote imewafikia wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya wasichana ya Jangwani na kutoa mafunzo ya kujenga uelewa kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita wapatao 250.

Akizungumza katika mafunzo hayo leo Oktoba 12, 2022 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Usalama Mtandao wa Wizara hiyo, Mhandisi Stephen Wangwe ametoa rai kwa wanafunzi hao kuwa makini kabla ya kutuma chochote ili kujikinga na uhalifu wa mtandaoni kama vile udhalilishaji, utapeli na udukuzi wa taarifa binafsi.

“Ni muhimu kuchukua tahadhali kwa kuacha tabia ya kutuma kila kitu mtandaoni na iwapo ikatokea umefanyiwa utapeli au viashiria vyovyote vya uhalifu wa mtandao inashauriwa kuripoti kituo cha polisi kilicho karibu kwa hatua stahiki kwa kuwa usalama wa mtandao huanza na mtu binafsi”, amesisitiza Mhandisi Wangwe.

Mhandisi Wangwe ameongeza kuwa elimu ya usalama mtandao ni muhimu sana ili watumiaji wa mitandao waweze kujilinda na athari zinazokuja na kukua kwa teknolojia ambapo wahalifu na wadukuzi nao hutumia teknolojia hiyo hiyo kufanya uhalifu na kugusa maisha ya watumiaji kwa kuharibu taswira na dira ya maisha yao.

Naye Mtaalamu wa Masuala ya Usalama Mtandao na Uchunguzi wa Kidijiti wa African ICT Alliance (AfICTA) kutoka Tanzania, Bw. Yusuph Kileo amewataka wanafunzi na vijana kutumia mitandao kwa uadilifu na kuzingatia usiri wa taarifa binafsi, na kuhakikisha namba za siri za akaunti zao ni imara, ngumu kutabirika na hazifanani.

Mwalimu Salum Kilipamwambu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani amesema licha ya somo ya TEHAMA kufundishwa shuleni hapo kulikuwa na umuhimu mkubwa kwa wanafunzi hao kujengewa uelewa kuhusu matumizi salama ya mtandao na kuwashukuru wataalamu wa Wizara kufika shuleni hapo.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi hao, Bi. Anna Ngowi mwanafunzi wa kidato cha sita amekiri kuwa elimu ya usalama mtandao imewapa majibu mengi ya nini cha kufanya kujilinda na uhalifu mtandaoni na kuahidi watakuwa mabalozi wazuri kwa wanafunzi na vijana wenzao.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi