Na Jacquiline Mrisho
Katika Mwaka wa Fedha 2018/19, uzalishaji wa zao la pamba umefikia tani 221,600 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 67 kutoka tani 133,000 zilizozalishwa mwaka 2017/18.
Takwimu hizo zimetolewa leo Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mhe. Omary Mgumba alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Igunga, Dkt. Dalaly Kafumu lililohoji ni lini Serikali itashughulikia changamoto za wakulima hasa kwa kupewa mbegu bure.
Mhe. Mgumba amesema kuwa mojawapo ya changamoto za wakulima wa pamba katika kuongeza tija na uzalishaji ni upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, wakulima kutotumia kikamilifu pembejeo pamoja na uzingatiaji wa kanuni za kilimo bora cha zao hilo.
Mhe. Mgumba amefafanua kuwa pamoja na changamoto hizo Serikali imeendelea kudhibiti ubora wa pembejeo kupitia Mamlaka mbalimbali ikiwemo Taasisi ya TPRI na Mamlaka ya Udhibiti wa ubora wa mbegu kwa kufanya majaribio ya mbegu za pamba kabla ya kupeleka kwa wakulima kwa ajili ya kupanda ili kuboresha uzalishaji wa zao hilo.
“Kutokana na mikakati ya Serikali katika kuboresha pembejeo hasa kwa kuelekeza wakulima kutumia mbegu aina ya UKM08 na iliyoondolewa manyoya kuanzia msimu wa 2018/19, uzalishaji wa pamba umeongezeka kufikia tani 221.600 kutoka tani 133,000”, alisema Mhe. Mgumba.
Mhe. Mgumba ameongeza kuwa utaratibu wa zamani haukuwa kuwapatia wakulima mbegu bure bali wakulima wa pamba waliwekewa utaratibu wa kukopeshwa kupitia Vyama Vikuu vya Ushirika na vya Msingi na kukatwa wakati wa kuuza pamba yao.
Aidha, mpango wa Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ili wakulima waweze kufanya shughuli zao kwa ufanisi na kupata faida ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa mitaji kwa ajili kwa ajili ya kuendeleza kilimo ikiwemo ununuzi wa pembejeo.
Vile vile, katika kuhakikisha wakulima wanapata pembejeo, Halmashauri ya Wilaya ya Igunga ilidhamini mkopo kwa wakulima kwa kutumia ushuru wake unaotokana na pamba ambapo wakulima hao walipata fursa ya kukopeshwa jumla ya shilingi 1,567,698,000 katika msimu uliopita.