Serikali imesema uwekezaji unaoendelea katika sekta ya anga umeanza kuzaa matunda, huku ukichochea ukuaji wa uchumi wa taifa na kuongeza mchango wake katika pato la taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 26, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema mchango wa sekta hiyo umeongeza pato la taifa kutoka asilimia 7.1 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 7.5 mwaka 2024.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo yenye thamani ya Shilingi Trilioni 1.154 kwa ajili ya kuboresha viwanja vya ndege, huduma kwa abiria pamoja na usafirishaji wa mizigo, hatua inayolenga kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri wa anga katika ukanda huu.

Miongoni mwa viwanja vya ndege vilivyoguswa na uwekezaji wa Serikali ni uwanja wa ndege wa Arusha , Moshi , Mwanza , Kagera , Msalato, Shinyanga , Tabora , Kigoma , Sumbawanga, Kabajwa na Serengeti katika Hifadhi ya Taifa Serengeti ambacho kipo katika hatua ya upembuzi yakinifu na usanifu wa miundombinu ya kiwanja cha ndege, usanifu wa jengo la abiria, jengo la mizigo na mfumo wa taa za kuongozea ndege.

Msigwa amesema maboresho hayo yameongeza mvuto wa Tanzania kwa mashirika ya kimataifa, ambapo mashirika saba mapya yameanza au kuonesha nia ya kutoa huduma nchini. Mashirika hayo ni Airlink, Zambia Airways, Saudia, Air France, Skyward Express, South African Airways na Xerin Air.
Amesema takwimu za mwaka wa fedha 2025/2026 zinaonesha ongezeko kubwa la idadi ya abiria na safari za ndege, hali inayochochea mapato ya kigeni na fursa za biashara. Serikali inatarajia kufikia zaidi ya safari 182,000 za ndege zitakazohudumia abiria zaidi ya milioni 6 kwa mwaka.

Aidha, Msigwa amesema Serikali imeendelea kuimarisha shirika la taifa kwa kununua ndege mpya, ambapo kwa sasa kuna jumla ya ndege 16 za masafa marefu na mafupi zinazohudumia safari za ndani na nje ya nchi.
Kwa sasa, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) inafanya safari katika vituo 33, kati ya hivyo 16 ni vya ndani na 17 ni vya kimataifa, hatua inayodhihirisha kupanuka kwa mtandao wa safari na kuimarika kwa ushindani katika sekta ya anga.


Amesisitiza kuwa uwekezaji huo una mchango mpana katika uchumi kwa kuongeza ajira, mapato ya kigeni na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama lango la biashara na utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki na kimataifa.