Kukamilika kwa ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa Msalato Jijini Dodoma kunatarajiwa kuupa nguvu mpya ya kiuchumi mkoa huo kupitia sekta ya anga. Mradi huo ni sehemu ya mpango mkakati wa Serikali ya awamu ya sita wa unaolenga kuwahudumia zaidi ya abiria milioni 1.5 kwa mwaka na kuongeza muunganiko wa safari za ndege kutoka ndani na nje ya nchi.
Kaimu Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato, Mhandisi Insubili Kabuka akizungumza katika mahojiano maalum na Idara ya Habari – MAELEZO ameeleza kuwa kukamilika na kuanza kutumika kwa uwanja huo kutaleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika Jiji la Dodoma.
“Uwanja huu wa kimataifa utawezesha muunganiko wa safari mbalimbali za ndege, kuimarisha uchumi na kuongeza hadhi ya Jiji la Dodoma kama Makao Makuu ya nchi. Hatujawahi kuwa na uwanja mkubwa wenye miundombinu ya kisasa kama huu,” amesisitiza Mhandisi Kabuka.
Amesema ujenzi wa uwanja huo unaendelea kwa kasi, na baadhi ya sehemu muhimu tayari zimekamilika akiongeza kuwa ili uweze kufanya kazi kikamilifu, sehemu za barabara za kuruka na kutua ndege, maegesho, pamoja na majengo ya abiria wanaoondoka na kuwasili lazima yakamilike.
Kwa upande wake Mhandisi wa mradi, Mahonda Luhende, amebainisha kuwa sehemu ya maegesho na kupaa/kutua ndege imekamilika kwa asilimia 95 ambapo kazi zilizobaki ni kuweka alama za uwanja na kufunga taa. Amesema Mkandarasi wa miundombinu na barabara anatarajia kukamilisha kazi ifikapo Mei 22, 2026, huku mkandarasi wa majengo akitarajia kumaliza Mei 27, 2026.
Uwanja huo, ukikamilika, unaotarajiwa kuwa daraja jipya la uchumi Dodoma, utaongeza usafirishaji wa ndege, kuimarisha biashara, na kuipa Dodoma fursa ya kipekee ya kushirikiana kimataifa. Serikali inasema uwanja huu sio tu kituo cha ndege, bali ni mlango wa maendeleo kwa mkoa mzima na taifa kwa ujumla.