Na Mwandishi Wetu Maalum Kisiwa cha Sal-Cape Verde
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masula ya Utalii Duniani (UNWTO) limeahidi kushirikiana na Tanzania katika kuweka mikakati bora ya kuwajengea uwezo watu waliopo katika sekta ya utalii nchini kuanzia mwezi juni 2022
Hatua hiyo inakuja kufuatia hali mbaya ya ugonjwa wa COVID kuidhoofisha sekta ya utalii nchini na Duniani kwa ujumla huku Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ikikadiriwa kupata hasara ya dola 4.8 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh. trioni 11) kwenye sekta ya utalii kutokana na janga la Corona huku watu milioni 21 wakikosa ajira
Akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro katika kikao cha pembeni mwa mkutano wa UNWTO wa 64 wa Kanda ya Africa ukilenga kufungua fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii hasa katika kipindi ambacho sekta ya utalii inachechemea kutokana na kushambuliwa na ugonjwa wa Corona Katibu Mkuu wa UNWTO Zurab Pololiskashvil amesema mafunzo hayo yatatolewa kwa Wadau wa Utalii na ili waweze kuendana na janga la Corona katika kuendesha shughuli za utalii nchini
Mkutano huo wa UNWTO wa 64 wa Kanda ya Afrika unafanyika kwa muda wa siku nne kuanzia jana katika kisiwa cha SAL nchini Cape Verde ambapo umewakutanisha mawaziri 30 wa utalii Barani Afrika ukilenga kujadili mustakabali wa utalii barani Afrika na Duniani kwa ujumla kufuatia uwepo wa janga la ugonjwa wa Corona
Kat Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo unaongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro akiwa na maofisa na Makamishna Uhifadhi kutoka TFS na TAWA, maofisa pamoja na Balozi wa Tanzani nchini Ufaransa Mhe, Samuel Shelukindo.
Aidha, Katika kikao hicho Katibu Mkuu amesema mafunzo hayo yatazilenga jamii zinazozunguka vivutio vya utalii ili kuzijengea uwezo wa kushiriki moja kwa moja katika shughuli za utalii nchini likiwa lengo ni kutengeneza ajira nyingi zaidi kupitia sekta hiyo.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu huyo amemueleza Waziri Dkt.Ndumbaro kuwa UNWTO iko mbioni kuandaa kalenda ya mwaka ya UNWTO ambapo Tanzania nayo itakuwepo ktk orodha hiyo ya kuendana na matukio yatakavyopangwa katika mkutano huo
Amesema moja ya kipaumbele cha UNWTO kwa sasa ni kuitangaza Tanzania na Africa kwa ujumla
Akizungumza katika kikao hicho cha ana kwa ana na Katibu Mkuu huyo, Dkt.Ndumbaro amesema mafunzo hayo yatatoa matumaini kwa Wadau wa Utalii nchini baada ya ugonjwa wa Corona kuwatikisa
Hata hivyo, Dkt.Ndumbaro amemueleza Katibu Mkuu huyo kuwa Tanzania ni nchi ya kwanza Afrika kwa kufanya vizuri katika shughuli za Uhifadhi lakini katika suala la kujitangaza na kutafuta masoko ya utalii imekiwa haifanyi vizuri hivyo ujio wa mafunzo hayo yataiwezesha Tanzania kufanya vizuri katika nyanja hiyo.
Aidha, Dkt.Ndumbaro amemualika Katibu Mkuu wa UNWTO, Zurabu Pololikashvil kuja kutembelea vivutio volivyopo Tz na kusisitiza kuwa ataambatana naye katika ziara hiyo ya kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini.