Na Lilian Lundo - MAELEZO
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea vishikwambi 200 kutoka ofisi ya UN WOMEN Tanzania kwa ajili ya zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.
Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Salum Kassim Ali amevipokea vishikwambi hivyo kwa niaba ya serikali, Julai 2, 2022, Ofisi za TAKWIMU zilizopo Jijini, Dar es Salaam.
"Tumepokea Vishikwambi 200 vyenye thamani ya dola za kimarekani 85,000 kutoka Ofisi ya UN WOMEN Tanzania. Vishikwambi hivi vitatumika kwa ajili ya kukusanya data katika zoezi la sensa ya watu na makazi Tanzania Bara na Zanzibar," alifafanua Salum.
Aliendelea kusema kuwa, sensa ya mwaka huu wamejipanga kutumia vifaa vya kidijitali ambapo jumla ya vishikwambi 205,000 vitahitajika kwa ajili ya zoezi la sensa ya watu na makazi Agosti, 23.
Aidha, amesema kuwa, zoezi la upokeaji wa vifaa hivyo litaendelea mpaka mwishoni mwa mwezi huu, ambapo kila baada ya siku watakuwa wakipokea vifaa hivyo na hivi karibuni wanatarajia kupokea vishikwambi 10,000.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi wa UN WOMEN Tanzania, Hodan Addou, amesema kuwa, ni matumaimi yao vishikwambi hivyo vitasaidia katika ukusanyaji wa data wa kidijitali sio tu kwa sensa ya watu na makazi, lakini vilevile katika tafiti mbalimbali zitakazozofanyika hapa nchini.
"Data ni muhimu katika kutunga sera, sheria, mipango, programu na bajeti kwa ajili ya kuwainua wanawake na wasichana nchini, vilevile ni muhimu katika kujua idadi ya wanawake waliopo nchini na kufanyia kazi upendeleo wa kijinsia" alifafanua Hodan.
Aidha, ameitakia taasisi ya TAKWIMU kila la heri na mafanikio katika zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23, mwaka huu.