Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Umeme wa SGR Kukamilika Mwishoni mwa Mei, 2020
May 13, 2020
Na Msemaji Mkuu

 

  • Tanesco Kutumia Bil.1.2 Kuboresha Umeme Kiwanda cha Sukari Mtibwa

Na Zuena Msuya, Morogoro.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amesema mradi wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme utakaotumika katika reli ya kisasa ya kuendesha treni inayotumia umeme umekamilika kwa zaidi ya asilimia 94 na utakamilika kwa asilia 100 mwishoni mwa mwezi Mei 2020.

Dkt. Kalemani alisema hayo mkoani Morogoro alipofanya ziara ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya njia ya kusafirisha umeme mkubwa na kusema kuwa ameridhishwa na kasi ya ujenzi huo.

Waziri wa Nishati alisema kukamilika kwa mradi huo kutachangia kwa kiasi kikubwa uchumi wa nchi kwa kuongeza mapato kwa kuwa umeme mwingi utakuwa ukinunuliwa kutoka Shirika la Umeme nchini (TANESCO), vilevile Shirika la Reli nchini (TRL) litapunguza gharama za kununua mafuta ya kuendeshea treni.

Njia hiyo ya umeme itapita katika vituo vinne vya njia ya treni ya kisasa ambavyo ni Pugu mkoani Dar es salaam, Ruvu mkoani Pwani, Kidugaro na Kingulwira mkoani Morogoro.

“Mradi huu utakamilika ndani ya muda uliopangwa kwa sababu tayari nguzo kubwa za umeme 450 kati ya 455 zinazotumika katika ujenzi wa njia hiyo zimekwisha jengwa na kusalia nguzo tano tu ambazo zinaendelea kujengwa ili kukamilisha ujenzi na kitakachofuata ni kusubiri kukamilika kwa reli yenyewe ili tuanze kufanya majaribio ya umeme huo”, alisema Dkt. Kalemani.

Alisema kuwa mradi huo ni wa kwanza kwa nchi za Afrika Mashariki ukifuatiwa na Kenya ambayo imepanga kuanza kuujenga mwaka 2021 na Uganda ambayo imepanga kuanza kujenga mwaka 2025.

Mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 72.6 na mkandarasi amekuwa akilipwa fedha zake kwa wakati.

Akiwa katika Kiwanda cha Sukari Mtibwa, Dkt. Kalemani alisema kuwa serikali imetenga shilingi Bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme utakaokuwa ukitumiwa na kiwanda cha sukari peke yake katika kuendesha shughuli za uzalishaji.

Njia hiyo ya umeme inayotarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita kuanzia mwezi Mei mwaka huu itasaidia kiwanda hicho kupata umeme wa kutosha kukidhi mahitaji ya kiwanda na ziada kwa zaidi ya miaka mitano ijayo.

“Kilichonileta hapa ni kuwajengea njia ya umeme wenu peke yenu, tumeshakaa na wataalam ili kumaliza tatizo hili, umeme hapa unatoka Msamvu takribani Kilomita 100 na unatumiwa na watu wengi, fedha tayari imekwishatengwa na ujenzi utaanza Mei 13, 2020 bila shaka mtatanua kiwanda hiki hapo baadaye,” alisema Dkt. Kalemani.

Kwa sasa kiwanda cha sukari Mtibwa kinapata Megawati 5 hadi 8 ambao pia wakati mwingine unakuwa na nguvu ndogo kutokana na kusafiri umbali mrefu na umekuwa ukikatika kusababisha uharibifu wa vifaa na kutokidhi mahitaji ya uzalishaji.

Kiwanda hicho kilijengwa mwaka 1954 na kuanza uzalishaji mwaka 1963, kinauwezo wa kuzalisha tani 200 hadi 350 za sukari kwa siku, matarajio ni kuzalisha tani 1000 kwa siku kwa kuwa wanafanya ukarabati na kuboresha miundombinu kiwanda hicho ikiwemo umeme.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi