Serikali imesema imeanza hatua za kujenga ukuta katika eneo la Nungwi Zanzibar kwa ajili ya kusaidia kuzuia maji ya bahari kuingia kwenye makazi kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema hayo wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo Februari 01, 2024.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nungwi, Mhe. Simai Hassan Sadiki aliyetaka kujua kama eneo hilo limekidhi vigezo vya kujengewa ukuta kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Khamisi alisema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza miradi ya ujenzi wa kuta katika fukwe mbalimbali za bahari Tanzania Bara na Zanzibar.
“Eneo ambalo linapaswa kujengwa ukuta limekidhi vigezo na lina kila sababu ya kufanyiwa hivyo, tumeanza kufanya utafiti na ndio maana viongozi wa SMT na SMZ wameshafika pale na tumeombea bajeti, hivyo Serikali ina kila sababu ya kulifanyia kazi eneo hilo,“ alisema.
Akijibu swali la msingi la mbunge huyo, Naibu Waziri Khamis alisema kuwa Serikali itaendelea kubaini maeneo yenye changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira na kuyaweka katika kipaumbele ili kuyatafutia rasilimali fedha kwa ajili ya kuitatua.
Akiendelea kujibu swali hilo amesema kuwa mabadiliko ya tabianchi yanazidi kusababisha athari katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya ukanda wa pwani nchini.
Katika kubainisha maeneo yaliyoathirika na kuyaweka katika vipaumbele, alisema Serikali inafanya tathmini ya kiwango cha uharibifu na athari zitakazojitokeza, hiyo ni moja ya sababu ya mojawapo ya vigezo vinavyotumika kuweka vipaumbele maeneo yaliyoathirika katika mipango ya utekelezaji
Kwa upande mwingine alitoa rai kwa wananchi kuacha kufanya shughuli zinazoharibu mazingira ya visiwa zikiwemo uvuvi usio endelevu na kilimo cha mwani kinachoharibu mazingira