Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ukusanyaji Mapato Halmashauri Waongezeka
Mar 11, 2025
Ukusanyaji Mapato Halmashauri Waongezeka
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akikabidhiwa mfano wa funguo leo Machi 11, 2025 Jijini Dodoma ikiwa ni ishara ya kumkaribisha jijini Dodoma kuwa mgeni rasmi wa Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT).
Na Mwandishi Wetu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezipongeza halmashauri kwa kuongeza ukusanyaji mapato na kudhibiti matumizi mabaya ya rasilimali za Serikali.

Mhe. Dkt. Samia ametoa pongezi hizo leo Machi 11, 2025 Jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 39 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa (ALAT).

“Niwapongeze halmashauri kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato, maono yangu ni kwamba mnaweza kufanya vizuri zaidi ya hapa. Nendeni kajipangeni tukusanye vizuri zaidi,” amesema Mhe. Rais.

Ameendelea kusema kuwa, udhibiti wa udokozi wa matumizi mabaya nao umeendelea kupungua, ambapo katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu ameona hakuna matukio ya kutoa hati mbaya kwa Serikali za Mitaa.

Aidha, amezitaka halmashauri kuongeza juhudi ya kufanya vizuri ili kuondoa kasoro ndogo ndogo zilionekana katika taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali.

Mhe. Rais amewataka viongozi wa ALAT, kusimamia vizuri suala la matumizi mabaya ya fedha za umma na ulegevu kwenye makusanyo ya mapato.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema Serikali imeonyesha kuwa maendeleo yanaanzia chini kwenda juu, kwa kuimarisha Serikali za Mitaa na kuwawezesha Wananchi kushiriki moja kwa moja katika mchakato wa maendeleo.

“Leo hii tunapozungumzia Serikali za Mitaa, tunazungumzia moyo wa maendeleo ya Wananchi. Serikali yako Mheshimiwa Rais imeonyesha kwamba mabadiliko ya kweli huanzia ngazi ya chini, ambako ndiko maisha ya Wananchi yanapoguswa moja kwa moja,” amefafanua Mhe. Mchengerwa.

Ameendelea kusema kuwa, ujenzi wa hospitali na vituo vya afya umeleta huduma za afya karibu na Wananchi na kuokoa maisha pamoja na kupunguza vifo vya wakina mama na watoto.

Aidha, uboreshaji wa barabara kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umeunganisha vijiji na masoko, ambako kumechochea biashara na kuinua uchumi wa wakulima.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi