Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ukarabati Kivuko cha MV Tanga Wafikia Hatua Nzuri
Sep 06, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Alfred Mgweno - TEMESA TANGA

Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme nchini (TEMESA) inaendelea na utekelezaji wa miradi ya ukarabati wa vivuko nchini ambavyo muda wake wa kukarabatiwa umefika ili viendeelee kutoa huduma vikiwa katika hali ya usalama, katika muendelezo huo, kivuko cha MV TANGA kinachotoa huduma kati ya Pangani na Bweni wilayani Pangani mkoani Tanga ni miongoni mwa vivuko ambavyo vinaendelea kufanyiwa ukarabati mkubwa

Akizungumza wakati akikagua maendeleo ya ukarabati wa kivuko hicho unaoendelea katika eneo la Pangani mkoani Tanga, Meneja wa Vivuko Kanda ya Mashariki na Kusini, Mhandisi Lukombe King’ombe amesema ukarabati huo unahusisha kuondoa mabati ambayo yameharibika sehemu za abiria na magari yanapopaki yakiingia ndani ya kivuko pamoja na chini ya kivuko, viti vya abiria, Kuweka vifaa vipya vya uokozi ikiwemo majaketi ya kujiokoa pamoja na maboya ya kujiokoa, kuondoa milango ya mbele na nyuma ya kivuko (ramps), kufunga viongoza kivuko vipya (navigation systems) pamoja na kupaka rangi kivuko hicho mara baada ya ukarabati wake.

 ‘’Mkandarasi yuko ndani ya muda wa utekelezaji wa mradi huu baada ya malipo ya awali na ameshaleta matirio zote za mabati yanayohitajika kwa ajili ya kubadilisha haya yaliyokwishakatwa, mabati haya yapo hapa eneo la mradi na tumetembea kuja kukagua na tunamuhamasisha Mkandarasi ili aweze nae kukamilisha hii kazi ndani ya muda mfupi ili kivuko cha MV.TANGA sasa kiweze kurudi kusaidiana na chenzie cha MV. PANGANI II ambacho kwa sasa ndo kinatoa huduma katika eneo la Pangani Bweni’’. Alimaliza Mhandisi King’ombe.

Naye Mkuu wa Kivuko cha Pangani, Mhandisi Abdulrahman Ameir akizungumza wakati wa ukaguzi huo ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kuboresha huduma za vivuko nchini kwa kuendelea kuvifanyia ukarabati vivuko vyake kote nchini na kuahidi kusimamia kwa ukaribu kuhakikisha mkandarasi anamaliza kukarabati kivuko hicho kwa ufanisi na katika muda uliopangwa na kukirejesha kivuko hicho kutoa huduma haraka iwezekanavyo.

Kwa mujibu wa Mkandarasi anayefanya ukarabati huo, Dar es Salaam Merchant Group, kivuko cha MV.TANGA kinatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Oktoba mwaka huu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi