Serikali imeshaanza usanifu wa barabara ya kuruka na kutua ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Kigoma kutoka mita 1,800 uliopo sasa hivi hadi kufikia mita 3,000 ili kuwezesha ndege kubwa kama vile Bombadier Q400 na Boeing kutua bila changamoto yoyote.
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Godfrey Kasekenya, amezungumza hayo mkoani Kigoma akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayoendelea.
“Tunategemea uboreshaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kigoma uanze mwaka huu wa fedha 2021/22 ambapo hadi sasa tupo katika hatua ya manunuzi kwa ajili ya kumpata mkandarasi”, amesema Naibu Waziri huyo.
Aidha, ameeleza kazi zingine zitazofanyika katika Kiwanja hicho ni ujenzi wa jengo la abiria, njia za ndege, sehemu ya maegesho ya ndege, mnara wa kuongozea ndege, jengo la zimamoto, barabara za kuingia na kutoka uwanja wa ndege na taa za kuongozea ndege wakati wa usiku.
Ameongeza kuwa lengo kuu la Serikali ni kufanya Kiwanja hicho kifanye kazi masaa 24.
“Lengo kubwa la Serikali ni kuufungua Mkoa wa Kigoma kwa njia ya anga, barabara, reli na maji”, amesisitiza Mhandisi Kasekenya.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Kasekenya amekagua ujenzi wa barabara ya Uvinza – Malagarasi (km 51.1), kwa kiwango cha lami na kusisitiza kwa Wakandarasi kuongeza vifaa, wafanyakazi pamoja na kupanga mpango kazi mpya wa kutekeleza miradi hiyo usiku na mchana.
“Barabara hizi tuzikamilisha tutakuwa tumemaliza changamoto ya vumbi kuanzia Kigoma, Uvinza, Urambo, Tabora hadi Manyoni na kuelekea hadi Mji wa Serikali wa Dodoma”, amefafanua Mhandisi Kasekenya.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Narcis Choma, ameeleza kuwa ujenzi wa barabara ya Uvinza - Malagarasi kwa kiwango cha lami unagharimu shilingi Bilioni 62 na utekelezaji wake ni miezi 24.
Ukamilikaji wa miradi hiyo ya kimkakati katika Mkoa wa Kigoma ni moja ya azma ya Serikali katika kufungua mkoa huo ambao ndio lango kuu la biashara kati ya Tanzania na nchi za DRC, Burundi na Rwanda.