Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ujenzi wa Kituo cha Huduma ya Pamoja Mpakani Wafikia Asilima 67
Aug 13, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Mradi wa ujenzi wa kituo cha huduma ya pamoja mpakani (OSBP) mpakani mwa Tanzania na Malawi eneo la Kasumulu unaojengwa na mkandarasi China Geo Engineering Corporation umefikia asilimia 67.1 na unatarajiwa kukamilika mwezi Septemba, 2021.

Hayo yamesemwa mkoani Mbeya na Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, mara baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa kituo hicho unaojengwa kwa awamu tatu na unagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 26.

“Nitoe wito kwa mhandisi mshauri kuusimiamia mradi huu kikamilifu ili ukamililike kama ulivyopangwa kulingana na mkataba”, amesisitiza Naibu Waziri huyo.

Aidha, Naibu Waziri Kasekenya amesema kuwa mpaka sasa mkandarasi hana madai yoyote anayodai yatakayokwamisha utekelezaji wa mradi huo.

Kwa upande wake, Mhandisi Mshauri wa Mradi kutoka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Mhandisi Daniel Mandari, amemueleza Naibu Waziri kuwa licha changamoto zilizoukabili mradi huo kuchelewa kukamilika, mkandarasi amekwisha kamilisha ofisi za wahandisi na maabara asilimia 100, ujenzi wa jengo la malori asilimia 80, Ghala asilimia 85, jengo la mifugo asilimia 84, jengo la abiria asilimia 81, geti namba 1&2 asilimia 75 na mizani asilimia 85.

Mhandisi Mandari ameongeza kuwa mkandarasi amekwishakamilisha kazi za uandaaji wa ushindiliaji matuta ya karibu barabara zote na kwa sasa anendelea kukamilisha miundombinu ya mabomba ya maji safi, taka, zimamoto kabla ya kuanza tabaka la lami.

Kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha huduma ya pamoja mpakani (OSBP) mpakani mwa Tanzania na Malawi katika eneo la Kasumulu kutakuza uchumi wa nchi zote mbili.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi