Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ujenzi Barabara Njombe-Ludewa Kurahisisha Uwekezaji Liganga na Mchuchuma
Dec 21, 2023
Ujenzi Barabara Njombe-Ludewa Kurahisisha Uwekezaji Liganga na Mchuchuma
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka akizungumza katika ukumbi wa mkutano wa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Wakurugenzi wa Halmashauri na Waandishi wa Habari leo tarehe 21 Desemba 2023 mkoani humo.
Na Jacquiline Mrisho MAELEZO

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka amesema kuwa ujenzi wa kipande cha barabara ya kutoka Lusitu hadi Mawengi wilayani Ludewa yenye urefu wa kilomita 50 iliyojengwa kwa zege ambayo tayari imekamilika na ujenzi wa kipande cha kutoka Nundu hadi Lusitu kinachoendelea kwa gharama ya shilingi bilioni 95 utarahisisha uwekezaji katika mradi wa Liganga na Mchuchuma uliopo wilayani humo.

Mtaka amefafanua kuwa, Serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na TANROADS pamoja na TARURA ambapo kama Mkoa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia kwa kusaidia mkoa kuweza kuzungumza kwa upande wa miundombinu ya barabara huku akitolea mfano miaka ya nyuma kutoka Njombe kwenda Makete ilikuwa ni safari ya masaa nane hasa kwenye hali ya mvua lakini leo Makete kunafikika ndani ya saa moja.

"Katika Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, inajengwa barabara ya zege ambayo huenda ndiyo barabara ghali zaidi kwenye ujenzi wa barabara Tanzania, ujenzi wa barabara hiyo ni matayarisho ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa Mchuchuma na Liganga, hivyo miundombinu itakuwa si sehemu ya uwekezaji bali Muwekezaji atajielekeza katika utekelezaji wa mradi moja kwa moja", alisema Mhe. Mtaka.

Mhe. Mtaka ametaja jambo lingine kubwa Rais Samia alilolifanya katika mradi huo kuwa ni kufanya maamuzi ya kulipa fidia ya shilingi bilioni 15 kwani mradi huo umekuwa kwenye mazungumzo ya Serikali kwa zaidi ya miaka 30 lakini Serikali haikuwahi kulipa fidia, hivyo ni kusudio la Rais Samia kuona mradi huo mkubwa unafanya kazi.

Vile vile, Mhe. Mtaka amesisitiza kuwa mradi huo ni muhimu na hata kwenye eneo la uchumi mpya katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo imezinduliwa hivi karibuni, imeutaja mradi huo ambapo utakapoanza kufanya kazi, utabadilisha uchumi wa nchi kwani dunia ipo kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda na viwanda vinategemea chuma na madini ambayo yanapatikana katika mradi huo. Aidha, ameendelea kukaribisha wawekezaji katika mradi huo.

Akizungumza kuhusu maendeleo mengine ya mkoa huo, amesema kuwa mkoa huo una vijiji 381 na vimebaki vijiji 30 ambavyo havijafikiwa na umeme ambapo mradi mwingine unaoendelea sasa ni wa REA kutoa umeme kwenye vijiji kwenda kwenye vitongoji ili kufikia 2025 zaidi ya asilimia 85 umeme uwe umefika kwenye vitongoji.

Katika Sekta ya Maji, mkoa una zaidi ya asilimia 75 ya upatikanaji wa maji mijini na vijijini ambapo kuna miradi mikubwa ya maji inaendelea katika Halmashauri za Wilaya za Makambako, Wangingombe na Njombe ambapo miradi hii ikikamilika kufikia mwaka 2025 maji yatapatikana kwa zaidi ya asilimia 90.

Mkoa huo pia unafanya vizuri katika kilimo ambapo maamuzi ya Rais Samia kuweka ruzuku kwenye mbolea yamekuwa ni maamuzi yenye tija katika mkoa huo kwani ni mkoa ambao wananchi wanazalisha kwa wingi. Vile vile, mkoa huo ni miongoni mwa mikoa iliyopokea fedha nyingi kwa ajili ya sekta ya elimu ikiwemo fedha za mradi wa SEQUIP, pia ni miongoni mwa mikoa ambayo imepata shule maalum inayoendelea kujengwa katika Halmashauri ya Wangingombe.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi