Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amempongeza na kumshukuru Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kwa kuwa miongoni mwa viongozi wanaoendeleza fikra za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ikiwa ni kielelezo cha kuendeleza uhusiano mzuri ulipo baina ya nchi mbili za Tanzania na Uganda.
Akizungumza leo Ikulu jijini Dar es salaam, akiwa pamoja na mgeni wake Rais wa Uganda Yoweri Museveni ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, aliyewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja, Rais Magufuli amemshukuru Rais Museveni kwa kuimarisha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.
“Namshukuru Rais Museveni anaendeleza uhusiano wetu wa nchi hizi mbili, nataka niwaambie uhusiano wa Tanzania na Uganda ni mzuri sana” alisema Rais Magufuli.
Rais Magafuli alitaja masuala kadhaa waliyozungumza kuwa nia ni kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili, ambapo alisema kuwa kwa sasa biashara ya usafirishaji wa mizigo kwa njia ya treni kati ya Uganda na Tanzania imerejea baada ya kusimama kwa takriba miaka 10 na mzigo wa kwanza uliosafirishwa ulikuwa na uzito unaolingana na semitrela 40 hadi 50.
Aidha, alisisitiza kuwa “utandawazi ni mzuri katika biashara, lakini ni lazima tuangalie kwa upana na sheria zetu zizuie changamoto zinazotokana na suala hilo”.
Akitolea mfano sukari ya ziada iliyoingizwa kinyemela katika masoko ya nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, ambayo haikutengenezwa nchini Uganda kama ilivyodaiwa hapo awali, Rais Magufuli alitahadharisha kuwa tatizo hilo linaweza kuuwa viwanda vya ndani, pamoja na kupoteza ajira kwa wazawa wa nchi hizo.
Kwa upande wake, Rais Museveni, ambaye amekuja nchini kwa lengo la kumweleza Rais Magufuli juu ya Mkutano wa Mataifa yanayoinukia kiuchumi (BRICS) uliofanyika mwezi uliopita huko nchini Afrika ya Kusini alisema kuwa aliwaelezea wafanyabishara wa nchi hizo juu ya fursa za uwekezaji zilizopo katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Ambapo, aliwataka wafanyabiashara hao kuja kuwekeza katika maeneo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara na treni.
“Nilipata heshima ya kuzikaribisha kampuni zao zije kuwekeza huku Afrika Mashariki, kwani zitapata faida, kwa vile kiwango cha faida watakachopata huku ni kikubwa kuliko Ulaya, Asia na Amerika ya kusini” alisema Rais Museveni
Aidha, Rais Museveni alitaja utalii kama eneo lingine alilowataka wafanyabiashara hao wa nchi za BRICS kuja kuwekeza na kuongeza kuwa atafufua Shirika la Taifa la Ndege la Uganda ikiwa ni katika jitihada za kuimarisha sekta hiyo katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki.
Kuhusu masuala ya kikanda baina ya nchi na za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Museveni alishukuru kuona Rais Magufuli amefufua usafirishaji wa mizigo kwa njia ya treni kutoka Dar es salaam hadi Mwanza na hatimaye kuvuka ziwa Victoria.
Aidha, alibainisha kuwa kusafirisha bidhaa kwa kutumia usafiri wa barabara ni gharama, kuliko kutumia usafiri wa treni, matokeo yake ni kuwa bidhaa zilizosafirishwa kwa barabara zinakuwa na gharama ya juu kuliko zile zilizosafirishwa kwa treni.
Vilevile alibainisha kuwa changamoto zilizopo katika nchi za Burundi na Sudani ya Kusini zinaendelea kupatiwa ufumbuzi, ikiwa ni pamoja na wakimbizi kutoka nchi ya Burundi kurudi katika nchi yao.
Rais Museveni alikuwa nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja ambapo, amerejea nchini Uganda mara baada ya kumaliza ziara yake.