Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeanza ziara ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa wote kwenye maeneo mbali mbali nchini ambapo wamekagua uwepo wa mawasiliano hayo kwenye eneo la kijiji cha Mkulazi kilichopo tarafa ya Ngerengere mkoa wa Morogoro ambapo Serikali imedhamiria kuwekeza na kujenga kiwanda cha sukari.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Moshi Selemani Kakoso akiongoza wajumbe wa Kamati yake, wamefika kwenye eneo hilo la uwekezaji na kudhibitisha uwepo wa mawasiliano. Kakoso ameushukuru Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kutekeleza azma ya Serikali ya kupeleka mawasiliano ambapo hamna mawasiliano na imewezesha nia ya Serikali ya kuwekeza kwenye viwanda.
Kakoso amewataka wananchi waitumie nafasi hii vizuri, minara inahitaji ulinzi ili rasilimali iliyowekwa iweze kufanya kazi muda wote. “Wananchi watambue mradi ni mali yao,” Kakoso amesema. Ameishukuru na kuipongeza UCSAF kwa kufanya kazi ya kufikisha huduma za mawasiliano kwenye maeneo ambayo hayana mvuto wa kibiashara kama haya ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za mawasiliano. Amefafanua kuwa eneo hili lina wakazi wachache lakini UCSAF imefikisha huduma za mawasiliano. Pia tumeshuhudia eneo hili lina wanafunzi wanasoma, nashauri UCSAF muwapatie vifaa vya TEHAMA ili kuwawezesha kusoma vizuri zaidi.
Naye Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amesema kuwa Serikali iliilekeza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuwekeza na kujenga kiwanda cha sukari katika eneo la Mkulazi lililopo Kata ya Mkulazi, tarafa ya Ngerengere mkoa wa Morogoro. Nditiye ameishukuru Kampuni ya simu ya Vodacom kwa kushirikiana na UCSAF kujenga mnara na kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi ambapo amekuta mawasiliano kweli yapo. “Mawasiliano ni uchumi na ni usalama”, Nditiye amesema. “UCSAF imefanya kazi kubwa sana, huku hakuna kampuni yeyote inaweza kujitokeza peke yake kuja kuwekeza mawasiliano kwenye eneo kama hili bila kupata ruzuku ya Serikali,” amesema Nditiye. Ameongeza kuwa, uwepo wa mnara huu utawawezesha wawekezaji kuwasiliana ndani na hata nje ya nchi.
Katibu Mtendaji wa UCSAF, Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa Mkulazi ni eneo ni jipya la uwekezaji ambapo linafanyiwa uwekezaji na mifuko ya hifadhi ya jamii ya PPF na NSSF na wamepewa eneo hilo na Serikali kujenga kiwanda cha sukari tangu mwaka 2016 ambapo walifika UCSAF na kuiomba ijenge na kufikisha huduma za mawasiliano kwenye eneo hilo kwa kuwa hapakuwa na mawasiliano ya aina yoyote. Katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa upande wa viwanda na uwekezaji wa kujenga viwanda, “sisi tulipokea ombi hilo na kuwasiliana na kampuni za simu ambapo Vodacom walikubali na walichukua ruzuku na kujenga mnara huo,” amesema Ulanga.
Amefafanua kuwa UCSAF tuliipatia Vodacom shilingi milioni 140 za kujenga mnara huo ambapo nao wenyewe Vodacom waliongeza fedha zao kwa kuwa ujenzi wa mnara huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 300. Mnara huu umeanza kufanya kazi tangu miezi miwili iliyopita ha hadi sasa una miezi minne tangu ulipoanza kujengwa.
Ulanga ameongeza kuwa tayari UCSAF imeshapokea maombi kutoka kwa wajenzi wa Stigglers Gorge ya kufikisha na kuboresha mawasiliano kwenye maeneo yao ya makambi ili kuwawezesha kupata huduma za mawasiliano wakati wa ujenzi wa mradi huo ili waweze kuwasiliana.
Mwakilishi wa Kampuni ya Vodacom kutoka Makao Makuu ya kampuni hiyo iliyopo Dar es Salaam Mhandisi wa Mawasiliano na Mipango Bwana David Mbogela amesema kuwa eneo hilo halikuwa na mawasiliano ya aina yoyote hapo awali ambapo wao wamejenga mnara huo kwa kushirikiana na UCSAF. Ameongeza kuwa mnara huo unatumia nishati ya umeme wa jua na jenereta ili kuhakikisha kuwa wananchi wanapata mawasiliano wakati wote kwa kuwa hakuna chanzo kingine cha nishati ya umeme.
Naye mwanakiji wa kijiji cha Mkulazi aishie maeneo hayo Bwana Naize Omary Uzuri ameishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuwawezesha kupata huduma za mawasiliano kwa kuwa katika kijiji chao tangu huduma za mawasiliano zianze kutumika nchini, kijiji chao hakijawahi kupata huduma hiyo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano