Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uchumi wa Bluu Wafungua Fursa Za Biashara Na Uwekezaji
Oct 07, 2026
Uchumi wa Bluu Wafungua Fursa Za Biashara Na Uwekezaji
Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, akizungumza na waandishi wa habari katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Na Scolastica Sambi

Tanzania imehimiza nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi kuendelea kushirikiana katika kutumia fursa za uchumi wa bluu kwa ajili ya kukuza biashara, uwekezaji na ajira, huku wakizingatia uhifadhi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.

Akizungumza Oktoba 7, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, wakati wa siku ya pili ya Mkutano wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi, Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa, amesema ukanda wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi una fursa nyingi zinazoweza kuchochea biashara na uwekezaji kupitia uchumi wa bluu.

Amesema fursa hizo zinapatikana katika maeneo mbalimbali, ikiwemo kilimo cha mwani, upandaji wa mikoko, ufugaji, usafirishaji wa mizigo kupitia bandari na vyombo vya baharini, utalii, michezo, uvuvi, uchimbaji wa madini na utafutaji wa nishati baharini.

“Fursa hizi za uchumi wa bluu zinatengeneza mnyororo mpana wa shughuli za kiuchumi katika bahari yetu. Ndiyo maana tumewakutanisha wafanyabiashara, wajasiriamali, mabenki na taasisi mbalimbali ili tuweze kuzijadili na kuona namna ya kuzitumia fursa hizi kwa ajili ya biashara na uwekezaji,” amesema.

Mhe. Kwagilwa amesema Tanzania imeainisha maeneo ya kipaumbele katika uchumi wa bluu, yakiwemo nishati, uvuvi, usafirishaji, utalii na michezo, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau katika kutumia fursa hizo kwa manufaa ya kiuchumi.

Amesisitiza kuwa matumizi ya fursa za uchumi wa bluu yanapaswa kwenda sambamba na uhifadhi wa rasilimali za bahari na mazingira yake, ili kuhakikisha rasilimali hizo zinatumika kwa uendelevu na kunufaisha kizazi cha sasa na kijacho.

Aidha, amezitaka nchi wanachama wa Mkataba wa Nairobi kuendelea kushirikiana katika uhifadhi wa bahari na matumizi endelevu ya rasilimali zake, kwa kuwa ikolojia na rasilimali za bahari huvuka mipaka ya nchi moja na hivyo zinahitaji juhudi za pamoja.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi

slot gacor