Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uchorongaji Visima vya Jotoardhi Kuanza Aprili 2024 - Dkt. Biteko
Feb 28, 2024
Uchorongaji Visima vya Jotoardhi Kuanza Aprili 2024 - Dkt. Biteko
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akizungumza baada ya kuwasili katika eneo lenye chanzo cha nishati ya jotoardhi katika Mji wa Naivasha, Kaunti ya Nakuru nchini Kenya.
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa kazi ya uchorongaji wa visima vya Jotoardhi nchini Tanzania itaanza mwezi Aprili mwaka huu ili kuweza kuhakiki rasilimali ya jotoardhi iliyopo kabla ya kuanza kwa shughuli za uzalishaji umeme kutokana na nishati hiyo.

 

 

 

Dkt. Biteko amesema hayo baada ya kutembelea vyanzo na mitambo ya kuzalisha umeme wa jotoardhi katika Mji wa Naivasha, Kaunti ya Nakuru nchini Kenya.

 

 

 

“Tumekuja kwenye mitambo ya kuzalisha umeme unaotokana na jotoardhi inayomilikiwa na kampuni ya uzalishaji umeme ya Kenya (KenGen) na tumejionea jinsi walivyopiga hatua kwenye uendelezaji wa rasilimali hii kwani tayari wanazalisha umeme wa Jotoardhi wa kiasi cha megawati zaidi ya 799.” Amesema Dkt. Biteko.

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko pamoja na viongozi wengine kutoka Tanzania wakikagua mitambo ya jotoardhi iliyopo katika Mji wa Naivasha, Kaunti ya Nakuru nchini Kenya (haipo pichani). 

 

Amesema Tanzania kwa upande wake, tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya kuendeleza vyanzo vya jotoardhi na kwamba kampuni ya KenGen mwezi Aprili mwaka huu itakuwa mkoani Mbeya kwa ajili ya kuanza uchorongaji vyanzo vya jotoardhi katika eneo la Ngozi na Kiejo-Mbaka kwa kushirikiana na kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).

 

 

 

Dkt. Biteko ameipongeza kampuni ya KenGen ya Kenya kwa hatua kubwa waliyofikia katika uendelezaji wa Jotoardhi ambapo zaidi ya asilimia 60 ya umeme nchini humo unatokana na nishati hiyo.

Mitambo ya umeme wa jotoardhi iliyo katika Mji wa Naivasha katika Kaunti ya Nakuru nchini Kenya.

 

 

Ametanabaisha kuwa, Tanzania imeamua kuongeza vyanzo vya uzalishaji umeme na sasa nguvu kubwa inawekwa kwenye kuendeleza miradi kama hiyo ya jotoardhi ili kupata umeme wa kutosha kwa ajili ya wananchi.

 

 

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Maendeleo ya jotoardhi katika kampuni ya KenGen, Peketsa Mangi amesema kuwa, nchi hiyo imekuwa na ushirikiano mzuri na Tanzania katika kuhakikisha nchi hizo zinafanikiwa katika uendelezaji wa jotoardhi.

 

 

 

Ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuipatia nafasi KenGen kufanya kazi kwa pamoja na wataalan kutoka TGDC ili kuchimba visima vya uhakiki wa rasilimali hiyo nchini na kueleza kuwa, kampuni hiyo ipo tayari kufanya kazi husika kwa mafanikio.

 

 

 

Viongozi walioambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati kwenye ziara hiyo ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya

Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Benard Kibesse na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi