Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Uboreshaji daftari la kudumu la wapiga Dar, kufanyika Machi 17-23, 2025
Mar 05, 2025
Uboreshaji daftari la kudumu la wapiga Dar,  kufanyika Machi 17-23, 2025
Mkurugenzi wa Uchaguzi toka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Bw. Ramadhan Kailima akizungumza leo Machi 05,2025 Jijini Dar es Salaam wakati akitoa mada kuhusu maandalizi ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa wadau wa Mkoa wa Dar es Salaam, kwenye mkutano wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, na wadau.
Na Grace Semfuko -MAELEZO

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Jacobs Mwambegele amesema, zoezi la kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga Mkoani Dar es Salaam, litafanyika kwa siku saba kuanzia Machi 17 hadi 23.

Amesema katika zoezi hilo vituo vitafunguliwa kuanzia saa mbili kamili asubuhi mpaka saa kumi na mbili jioni na kuwataka wananchi kwenda kuhakiki taarifa zao pamoja na kujiandikisha.

Akizungumza wakati akifungua mkutano wa Tume hiyo na Wadau wa Uchaguzi, kuhusu uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Jaji Mwambegele amesema, kwa sasa tume imeanza maandalizi ya mzunguko wa 13 ambao ni wa mwisho wa uboreshaji wa daftari hilo unaohusisha Mkoa wa Dar es Salaam.

"Kwa mujibu wa ratiba, kwa sasa tume imeanza maandalizi ya mzunguko wa 13 na wa mwisho wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura hapa Mkoani Dar es Salaam, zoezi hili kwa hapa litafanyika kwa siku saba kuanzia Machi 17 hadi 23 mwaka huu wa 2025, na vituo vitafunguliwa kuanzia saa mbili kamili asubuhi mpaka saa kumi na mbili kamili jioni" amesema Mhe. Jaji Mwambegele.

Mhe. Mwambegele amewakumbusha wananchi kuwa, kujiandikisha kwenye daftari hilo zaidi ya mara moja ni kosa la jinai ambapo mtu yeyote atakaebainika kufanya hivyo akitiwa hatiani adhabu yake ni faini isiyopungua laki moja hadi laki 3, au kifungo cha miezi sita hadi miaka miwili

"Napenda niwakumbishe, kujiandikisha kwenye daftari zaidi ya mara moja ni kosa la jinai, ukifanya hivyo adhabu yake ni faini isiyopungua laki moja hadi laki 3, au kifungo cha miezi sita hadi miaka miwili au vyote kwa pamoja, hivyo niwaombe wananchi kujiepusha na kosa hili" amesema Mhe. Jaji Mwambegele.

Amesema tangu kuzinduliwa kwa uboreshaji wa daftari hilo Julai 20, 2024 Mkoani Kigoma, tayari mikoa 28 imeshakamilisha zoezi hilo ikiwepo mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara na Simiyu.

Mikoa mingine ni pamoja na Manyara, Dodoma, Singida, Arusha, Kilimanjaro, Mbeya, Iringa, Rukwa, Songwe, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara na Pwani pamoja na mikoa ya Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba na Kaskazini Pemba.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi