Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ubora Miundombinu ya Utalii Waongeza Idadi ya Watalii Nchini
Feb 26, 2026
Ubora Miundombinu ya Utalii Waongeza Idadi ya Watalii Nchini
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa akitoa Taarifa kwa na Vyombo vya Habari kuhusu Mafanikio ya Serikali katika sekta ya Usafirishaji, katika Mkutano uliofanyika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere , jijini Dar es Salaam.
Na Baraka Messa – MAELEZO

Serikali imesema sekta ya utalii nchini inaendelea kukua kwa kasi, ikionesha mwelekeo chanya katika ongezeko la watalii na mapato yatokanayo na shughuli za utalii kufuatia uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya utalii uliofanywa na Serikali katika maeneo ya hifadhi.

Akizungumza na vyombo vya habari leo  Februari 26, 2026 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema mafanikio hayo yametokana na maboresho ya miundombinu ya usafiri wa anga, reli ya kisasa ya SGR, ununuzi wa ndege mpya za kisasa za abiria na mizigo pamoja na mikakati madhubuti ya kuitangaza Tanzania kimataifa.

Amesema takwimu za mwaka 2024 na 2025, zinaonesha kuwa watalii wa nje waliongezeka kutoka 2,141,895 hadi 2,294,495, huku watalii wa ndani wakiongezeka kutoka 3,218,352 hadi 3,610,960. Hivyo, jumla ya watalii iliongezeka kutoka 5,360,247 mwaka 2024 hadi 5,905,455 mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 10.2.

“Kwa upande wa mapato, sekta ya utalii imeonesha mafanikio makubwa zaidi kwa kupanda kutoka dola za Marekani milioni 1.3 mwaka 2021 hadi dola milioni 3.9 mwaka 2024,” amesema Msigwa.

Amefafanua kuwa katika kuimarisha taswira ya Tanzania kimataifa, filamu ya Tanzania: The Royal Tour iliyoasisiwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na kampeni mbalimbali za kimataifa zimechangia kwa kiasi kikubwa kuvutia watalii na wawekezaji zaidi huku Tanzania ikifanikiwa kunyakua tuzo za utalii za dunia za “World Travel Awards” ikiwa ni muendelezo wa mafanikio baada ya kung’ara katika ngazi ya mabara.

Msigwa ameongoza kuwa Tanzania imetangazwa mshindi wa kipengele cha ‘Nchi Bora kwa Safari Duniani (World’s Leading Safari Destination 2025)’ ikiwa ni ushindi wa mara ya tatu mfululizo kuanzia mwaka 2023.

Aidha, Hifadhi ya Taifa Serengeti imefanikiwa kutwa tuzo ya Hifadhi Bora Zaidi Duniani (World’s Leading National Park 2025) na kuandika historia kwa kutwaa kwa mara ya kwanza tuzo hiyo.

Amesema mafanikio hayo yanaonesha wazi kuwa Tanzania imeendelea kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha utalii barani Afrika na duniani kwa ujumla. “Ushindi huu wa tuzo za kimataifa umeongeza hadhi ya nchi, kuimarisha imani ya watalii na wawekezaji, na kuchochea zaidi ukuaji wa sekta ya utalii ambayo ni mhimili muhimu wa uchumi wa taifa,” ameeleza Msigwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi