Ubelgiji imesema inaunga mkono kampeni ya Nishati Safi ya kupikia na hivyo imeonesha nia ya kushirikiana na Tanzania katika matumizi ya nishati hiyo kwa maendeleo ya bara zima la Afrika iliyoasisiwa na Kinara wa Kampeni hiyo Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Hayo yamebainishwa katika Kikao cha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko na Waziri wa Nishati wa Ubelgiji, Mhe. Tinne Van Der Straeten kilichofanyika mjini Windhoek, Namibia ikiwa ni sehemu ya Mkutano wa Nchi za Afika kujadili matumizi ya Hydrojen kutumika katika kuzalisha umeme.
Dkt. Biteko amesema ili kupata maendeleo ya kweli, Tanzania inatoa kipaumbele katika matumizi ya nishati ambayo itawawezesha kupata maendeleo endelevu ikiwa ni pamoja na kuondokana na magojwa na vifo vinavyotokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi.
Amesema ushirikiano wa miaka mingi kati ya Tanzania na Ubelgiji utawezesha upatikanaji wa maendeleo yanayoweza kutokana na uwekezaji wa kimkakati kutoka kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
“Kama mnavyofahamu, Tanzania kupitia Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeasisi na inaendeleza kampeni kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia katika kipindi cha miaka 10 ijayo kuanzia mwaka huu”, amesema Dkt. Biteko na kuongeza kuwa Tanzania ingetamani kuungwa mkono na Ubelgiji katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kama ambavyo imekuwa ikifanya katika sekta nyingine ikiwemo elimu na uwezeshaji katika masuala ya usawa kijinsia.
Kwa upande wake, Waziri Tinne amesema nchi yake iko tayari kuunga mkono jitihada za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwa ni mkakati wa kimataifa wa uhifadhi wa mazingira na kuwawezesha wananchi kukuza pato na maendeleo ya kiuchumi.
Amesema matumizi ya vyanzo mbalimbali vya nishati safi ni njia mojawapo ya kuchochea maendeleo ya watu na uchumi wa nchi husika.
Mkutano wa Hydrojen unaoendelea nchini Namibia unalenga kuibua fursa na changamoto zilizopo katika matumizi ya nishati hiyo ambapo Tanzania itapata fursa ya kujifunza kuhusu matumizi ya Hydrojeni kwenye upande wa kuzalisha umeme.
Mkutano wa Hydrojen unaohudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka nchi za Afrika unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 5 Septemba, 2024.