[caption id="attachment_53289" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akiangalia samaki aina ya Sangara wanaopatikana Ziwa Victoria.(Picha kutoka Maktaba)[/caption]
Na Jacquiline Mrisho - Dodoma
Uanzishwaji wa Kanda Kuu za Ziwa Victoria, Tanganyika na Pwani umesaidia kuimarisha ulinzi na usimamizi wa rasilimali za uvuvi pamoja na kudhibiti matumizi ya zana haramu.
Hayo yamebainishwa jana Bungeni, jijini Dodoma na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli wakati akilivunja Bunge la 11 ambapo amesema kutokana na hatua hizo mafanikio makubwa yamepatikana.
Rais Magufuli amesema kuwa kutokana na uanzishwaji wa kanda hizo Serikali imefanikiwa kuongeza uzalishaji wa sangara kwenye Ziwa Victoria kutoka tani 417,936 mwaka 2016 hadi tani 816,964 mwaka 2020 ambapo urefu wa sangara umeongezeka kutoka wastani wa sentimeta 16 hadi sentimeta 25.2.
“Hatua hizo zimeweza kupandisha mauzo ya samaki wetu nje ya nchi kutoka wastani wa shilingi bilioni 379 mwaka 2015 hadi shilingi bilioni 692 mwaka 2019, haya sio mambo madogo”, alisema Rais Magufuli.
Ameendelea kufafanua kuwa idadi ya wafugaji samaki pia imeongezeka kutoka 18,843 mwaka 2015 hadi 26,474 mwaka 2020, kuongezeka kwa idadi ya mabwawa kutoka 22,545 hadi 26,445, kuongezeka kwa vizimba vya kufugia samaki kutoka 109 hadi 431 na uzalishaji wa vifaranga kutoka 8,090,000 hadi 14,531,487.
Ili kuongeza tija katika sekta ya uvuvi, Serikali imeipa Benki ya Maendeleo Kilimo Tanzania (TADB) shilingi bilioni 324.8 na hivyo kuiwezesha Benki hiyo kutoa mikopo ya moja kwa moja kwa wakulima, wafugaji na wavuvi yenye thamani ya shilingi bilioni 166.9 kwa riba nafuu.