Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tutaendelea Kuenzi Uhusiano wa Kidini na Kiutamaduni na Uganda - Majaliwa
Dec 17, 2022
Tutaendelea Kuenzi Uhusiano wa Kidini na Kiutamaduni na Uganda - Majaliwa
Na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kuenzi uhusiano wa kidini na kiutamaduni kati yake na Uganda.

Amesema hayo leo Jumamosi (Disemba 17, 2022) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maadhimisho ya miaka 75 tangu ulipojengwa msikiti wa kwanza katika Chuo Kikuu cha Makerere kilichopo Kampala nchini Uganda. Msikiti huo ulifunguliwa na Mwanamfalme Abdullah wa Zanzibar mwaka 1948.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa  ujenzi wa msikiti huo umekuwa ni chachu ya kuimarisha mahusiano ya enzi kati ya wananchi wa Uganda, Zanzibar na iliyokuwa Tanganyika.

“Nyote mtakubaliana nami kwamba uwepo wetu hapa ni ishara tosha ya kutambua umuhimu na mchango wa tukio hili la kihistoria katika kukuza mahusiano ya watu wetu hususan ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki”

Aidha, Waziri Mkuu ameishukuru Serikali ya Uganda na Chuo Kikuu cha Makerere katika kuusimamia msikiti huo sambamba na kuruhusu Waislamu wa maeneo ya jirani kuutumia kwa ajili ya kuabudu.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa ametoa  rai kwa viongozi wa dini kuendelea kukemea mmomonyoko mkubwa wa maadili ambao umeshika hatamu.

“Katika hili ningeomba turejee maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Qur‘an tukufu Sura ya 33 Ayah 21 (Quran 33:21) kwamba “Hakika ninyi mnacho kiigizo chema kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu”.

Ameongeza kuwa taasisi za elimu, jumuiya za dini, viongozi wa dini na viongozi wa umma wanao wajibu wa kuilea jamii kwa kutoa elimu sahihi ya mazingira sambamba na mafundisho sahihi na endelevu ya dini ili kuiwezesha kutambua na kufuata yote yaliyomema kama tulivyo amrishwa na Mwenyezi Mungu na kuacha kabisa yote mabaya yanayomchukiza Mwenyezi Mungu.

“Nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wa Jumuiya kuongeza juhudi katika kutoa mafunzo ya dini ili kuijengea Jamii hofu ya Mwenyezi Mungu dhidi ya maovu na hivyo, kupunguza au kuondoa kabisa mmomonyoko wa maadili tunaoushuhudia sasa”

Awali Akizungumza katika maadhimisho hayo, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Makerere alisema kuwa Prof. Umaru Kakumba alisema kuwa ujenzi wa msikiti huo ulilenga kujenga maadili mema miongoni mwa wanachuo.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi