Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amesema Serikali inaendelea kufanya mageuzi makubwa yanalenga kuondoka kero za maji katika maeneo mbalimbali kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ya usambazaji wa maji na uanzishaji wa Gridi ya Taifa ya Maji itakayotumia vyanzo vya maji kutoka maeneo mbalimbali nchini
Mhe. Aweso amesema hayo Januari 28, 2026 Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya sekta ya maji katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa muhula wa pili wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema Serikali imekamilisha miradi mbalimbali ya maji ambayo sasa inahudumia wananchi ikiwemo ya Ziwa Victoria, miradi ya maji ya Musoma, Rorya-Tarime, Bunda, Simiyu, Mwanza, Geita, Chato, Biharamulo na Bukoba huku ikikamilisha usanifu wa mradi wa kutoa maji ziwa Victoria kwenda Jijini Dodoma kupitia Singida ambapo amesema taratibu za kupata makandarasi wa ujenzi zinaendelea.
Kwa upande wa Ziwa Tanganyika, Mhe. Aweso amesema Serikali imempata mtaalam mshauri kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa miradi ya kutoa maji kwenye ziwa hilo kuyapeleka kwenye mikoa ya Kigoma, Katavi, Songwe na Rukwa na taratibu za kimkataba zinaendelea.
Kuhusu kupeleka maji ya Ziwa Nyasa katika mikoa ya Njombe na Ruvuma amesema utaratibu wa kupata mtaalam mshauri unaendelea ambapo pia amesema utekelezaji wa miradi kwenye mito mikubwa ikiwemo Rufiji ambao unahusisha kupeleka maji Jijini Dar es Salaam, Pwani na Lindi na mto Ruvuma kwa ajili ya kupeleka maji katika Manispaa ya Mtwara-Mikindani upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo umekamilika.

Aidha, amesema Serikali imekamilisha miradi mikubwa ya maji 16 yenye thamani ya shilingi bilioni 16.28 pia inaendelea na utekelezaji miradi 71 yenye thamani ya shilingi bilioni 142.8 itakayonufaisha watu wapatao 2,887,029 ambapo amesema baadhi ya miradi hiyo imeanza kutoa huduma ikiwemo mradi wa maboresho ya miundombinu ya maji Mtwara mjini na uboreshaji wa miundombinu ya majisafi Jiji la Tanga Awamu ya Tatu.
Miradi mingine ni ya ukarabati na upanuzi wa Kituo cha kusukuma Maji cha Mabayan; mradi wa Nzuguni Awamu I Dodoma Mjini; Mradi wa ujenzi wa Miundombinu ya kutibu majitaka katika mji wa Igunga; mradi wa maji wa Mkinga–Horohoro, mradi wa maji wa Kigamboni katika Jiji la Dar Es Salaam na mradi wa maji wa Tunduma utakaogharimu shilingi bilioni 119 ambao Serikali imeshatoa malipo ya awali shilingi bilioni 5.99.

Katika hatua nyingine Mhe. Aweso amesema Serikali kupitia Wizara ya Maji inaendelea na zoezi la ununuzi na ufungaji wa dira za maji za malipo kabla 2,271 ambazo zitawawezesha wananchi kutumia maji kadri wanavyolipia pia kuondoa malalamiko ya wateja ‘’ kubambikiwa bili za maji ".