Na. Projestus Binamungu - WUSM
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa ameliagiza Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF) kushirikiana na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuhakikisha wanaiwekea mazingira wezeshi timu ya Taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 20.
Tanzanite yatakayowajenga kimwili na kisaikolojia wachezaji hao katika kuikabili timu ya taifa ya Ethiopia Januari, 2022.
Waziri Bashungwa ametoa agizo hilo Desemba 21, 2021 alipokutana nao na kufanya mazungumzo na wachezaji pamoja na kamati ya ufundi ya timu hiyo kujadili na kufanya tathimini ya changamoto mbalimbali za kimichezo zilizojitokeza wakiwa nchini Burundi wakati wa mchezo baina ya Tanzanite na wenzao wa timu ya wanawake ya Burundi ya chini ya umri wa miaka 20.
Waziri Bashungwa amesema kazi ya Serikali katika sekta ya michezo ni kuweka mazingira wezeshi kwa wanamichezo na timu zote zinazoipeperusha bendera ya taifa, na ndoto ya Serikali ni kuwaona wachezaji na timu zao wakiibuka washindi katika michezo yote.
Pamoja na kuelezea matamanio hayo ya Serikali, Waziri Bashungwa ameipongeza timu ya Tanzanite katika mchezo wao dhidi ya Burundi uliochezwa Desemba 18, 2021 na kuibuka na sare ya bao moja licha ya kucheza wakiwa pungufu.
“Kwa kweli mliishangaza Afrika na dunia huko Burundi, yaani mnacheza pungufu lakini bado tukapata ushindi wa heshima, kwa kweli tunawapongeza sana vijana wetu”, amesema Waziri Bashungwa.
Awali, akielezea baadhi ya changamoto walizokabiliana nazo huko Burundi, Mkuu wa msafara wa timu ya Tanzanite, Bukuku Mrisho amesema, licha ya sheria za mpira kutaka majibu ya vipimo vya magonjwa mbalimbali kuwasilishwa masaa mawili kabla ya mchezo lakini wao waliletewa majibu ya vipimo vya Uviko 19 wakiwa uwanjani tayari na hata wakati mchezo ukiendelea wataalamu waliendelea kuleta majibu ya vipimo kwa viongozi mbalimbali wa timu.
“Yaani wakati mchezo unaendelea waliendelea kutuletea makaratasi waliyo ya kuandikwa kwa mkono kwamba fulani majibu yanaonesha ana Uviko 19, sisi tunaamini nia yao ilikuwa ni kututoa mchezoni lakini tulipambana na upungufu wetu huo huo mpaka mwisho wa mchezo tukaibuka na sare ya goli moja” amesema Mrisho.
Tanzinite inashiriki michezo hiyo ya awali kupata tiketi ya kufuzu kushiriki mashindano ya kombe la dunia yanayotarajiwa kufanyika mwaka 2022 nchini CostaRica .