Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tuna Kila Sababu ya Kujivunia Muungano - Rais Samia
Apr 26, 2024
Tuna Kila Sababu ya Kujivunia Muungano - Rais Samia
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwasili na kukagua gwaride maalumu la maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hafla iliyofanyika Uwanja wa Uhuru leo Aprili 26, 2024 jijini Dar es salaam
Na Lilian Lundo, Maelezo

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuna kila sababu ya Watanzania kujivunia muungano, kwani umetokana na maamuzi ya Watanzania wenyewe.

Mhe. Dkt. Samia amesema hayo leo Aprili 26, 2024 wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zilizofanyika uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

“Tuna kila sababu ya kujivunia muungano wetu. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetokana na maamuzi yetu wenyewe, tuna makabila zaidi ya 120, imani za dini tofauti tofauti lakini tunaunganishwa na lugha moja ya Kiswahili. Tumeitunza na kuilinda nchi yetu kwa kudumisha amani na utulivu. Tuna kila sababu ya kujivunia muungano wetu,” amesema Mhe. Dkt. Samia.

Ameendelea kusema kuwa, katika kuendeleza muungano, Watanzania hawana budi kuitekeleza falsafa ya maridhiano, kustahimiliana, kuleta mageuzi na kujenga nchi, kwani italeta maendeleo endelevu katika nchi ili kufikia uchumi wa kati ngazi ya juu.

Aidha, Mhe. Rais ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii na maarifa zaidi ili kukuza tija kwa ustawi wa taifa, kwani kazi ndiyo kipimo cha utu.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya Tanzania akiwemo Mhe. Evariste Ndayishimiye, Rais wa Jamhuri ya Burundi; Mhe. Azali Assoumani, Rais wa Umoja wa Comoro; Mhe. Hakainde Hichilema, Rais wa Jamhuri ya Zambia na Mhe. Felix Tshisekedi, Rais wa Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Viongozi wengine ni Mhe. Hassan Sheikh Mohamud, Rais wa Shirikisho la Somalia; Mhe. William Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya; Mhe. Nangolo Mbumba, Rais wa Jamhuri ya Namibia; Mhe. Saulos Chilima, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Malawi; Mhe. Jessica Alupo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Uganda; Mhe. Adriano Maleiane, Waziri Mkuu wa Msumbiji na Mhe. James Kabarebe, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi