Serikali imeitaka Kamati ya Uwezeshaji wa Usafiri wa Anga kushauri matumizi ya teknolojia za kisasa katika uendeshaji wa usafiri wa anga nchini ili kuufanya kuwa na tija na rafiki kwa watumiaji nchini.
Akizungumza wakati akifungua kikao cha 51 cha kamati hiyo jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Bw, Gabriel Migire amesema usafiri wa anga umekuwa wa ushindani hivyo ni wajibu wa kamati hiyo kuhakikisha inakuja na mikakati ya kuwezesha usafiri huo kuwa katika hali nzuri.
“Teknolojia inakuwa kwa kasi sana na nyinyi kama wataalam mnatembea sasa sisi tusiwe tofauti na wengine kumbukeni usafiri wa anga una ushindani sana kuanzia kwenye kutoa huduma mpaka kwenye uendeshaji hivyo tukijifungia hatutapiga hatua’ amesema Katibu Mkuu Migire.
Katibu Mkuu Migire ameitaka kamati hiyo kutembelea kiwanja cha ndege cha Dodoma ili kuona miundombinu na huduma zinazotolewa ili kushauri maboresho stahiki yanayohitajika kwani kwa sasa Dodoma ni Makao Makuu ya nchi.
Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Migire ameitaka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzanaia (TAA), kuweka mikakati ya kujiendesha kibiashara ili kuboresha miundombinu kwa kutumia fedha za ndani.
“TAA hakikisheni mnapanga mikakati bora ya kujiendesha kibiashara kama KADCO, ili kuweza kujiendesha kibiashara na hivyo kusaidia uendeelezaji wa miundombinu kwa haraka,’ amesema Katibu Mkuu Migire.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw, Hamza Johari amesema pamoja na Changamoto zilizopo za Uviko 19, TCAA imeendelea kuhakikisha inasimamia usafiri huo ili kuhakikisha kunakuwa na usalama.
Bw, Johari ameongeza kuwa mpaka mwezi Aprili 2022 safari za ndege nchini zimeendelea kuongezeka na kufikia 113 kwa wiki ikilinganishwa na safari ambazo zilikuwa chini ya 50 mwezi Aprili mwaka 2021.
Kikao hicho cha wataalam wa uwezeshaji usafiri wa anga kinahusisha wadau wote wanaofanya kazi katika viwanja vya ndege nchini na hukutana mara mbili kila mwaka kujadili changamoto za uendeshaji wa viwanja vya ndege nchini.