Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tumieni Taasisi za Dini Kupambana na Dawa za Kulevya
Feb 26, 2025
Tumieni Taasisi za Dini Kupambana na Dawa za Kulevya
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza viongozi mbalimbali pamoja na Waumini wa dini ya Kiislam (hawapo pichani) mara baada ya kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa uliopo Tanga mjini tarehe 26 Februari, 2025.
Na Grace Semfuko, MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema taasisi za dini ni muhimu katika kukuza maadili na hivyo kuiomba jamii kutumia taasisi hizo katika kupinga matumizi ya dawa za kulevya.

Amesema kundi kubwa la vijana ndio linaloathirika zaidi na dawa hizo, hivyo endapo taasisi hizo zitasimama imara katika kutoa elimu, zitasaidia kuokoa kundi kubwa la vijana kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya ambao vijana hao ndio wanaotegemewa na Taifa.

Mheshimiwa Rais ametoa rai hiyo leo Februari 26, 2025, mara baada ya kuweka Jiwe la Msingi la upanuzi wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa uliopo Tanga Mjini.

"Ndugu zangu taasisi hizi za dini ni taasisi muhimu sana katika kukuza maadili, naomba tuzitumie katika kukuza maadili ikiwepo kupinga matumizi ya dawa za kulevya na mambo mengine yanayotokea huku kwetu. Tuna mipango mikubwa sana kwa mkoa huu wa Tanga, na kama mipango hiyo itakuta vijana wameshaathirika na dawa za kulevya, basi haitakuwa na maana kwa mkoa wetu," amesema Rais Samia.

Amewaomba wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kupambana na biashara ya dawa za kulevya inayoathiri vijana na hivyo kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi