Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tumieni Misingi ya Taaluma ya Uandishi, Uhuru Una Mipaka - Dkt. Tulia
May 02, 2024
Tumieni Misingi ya Taaluma ya Uandishi, Uhuru Una Mipaka - Dkt. Tulia
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson akizindua maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ya Dunia leo Mei 2, 2024 ambapo rasmi kilele chake kitakuwa Mei 3, 2024 na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi.
Na Georgina Misama – Maelezo

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Mabunge ya Dunia, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amewaasa waandishi wa habari kutumia misingi ya taaluma yao katika kutumia uhuru wa vyombo vya habari.

Dkt. Tulia alisema hayo leo Mei 02, 2024 jijini Dodoma wakati akizundua maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ya Dunia (WPFD), ambapo wadau wa habari kutoka ndani na nje ya Tanzania wakiongozwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wamekutana kwa siku tatu kujadili masuala ya kihabari.

Akitoa hotuba yake ya ufunguzi, Dkt. Tulia alisema wakati mijadala mbalimbali inaendelea katika maadhimisho hayo, ni vizuri kutafakari ukomo wa uhuru wa vyombo vya habari hususan katika kipindi hiki ambapo vyombo vya habari vina nafasi ya kubeba ajenda mbalimbali za kitaifa likiwemo suala la mazingira na mabadiliko tabianchi.

“Kuhusu uhuru wa vyombo vya habari, uhuru huu uwe na mipaka, tumieni misingi ya taaluma ya habari katika uandishi mkizingatia miiko ya uandishi wa habari mnazowapelekea wananchi, msiweke mawazo yenu wenyewe katika uhabarishaji,” alisema Mhe. Dkt. Tulia.

Aliongelea pia kuhusu uandishi wa ukatili wa kijinsia ambapo aliwataka waandishi kuandika kuhusu wanaume pia badala ya kuegemea kwa wanawake na watoto peke yao bali wahamasishe na kufundisha kwamba makundi yote katika jamii yanapaswa kuwa salama aidha, waibue changamoto zilizopo kwenye jamii ili viongozi wa serikali waweze kuzishughulikia kwa manufaa ya jamii kwa ujumla.

Vilevile, Dkt. Tulia aliongelea changamoto ya kiuchumi inayovikabili vyombo vya habari hususan madeni kwa serikali ambapo alisema taasisi zinazodaiwa na vyombo vya habari zinapaswa kujitathmini na kuwalipa wahusika mara moja na kwamba hatua hiyo itapelekea waandishi wa habari kwenye vyombo husika kulipwa mishahara yao inayokidhi hali na kwa wakati.

Dkt. Tulia pia alizungumzia suala la waandishi wa habari za Bunge na kuwataka wahariri wa vyombo vya habari kuchagua waandishi maalum wa kuripoti masuala ya Bunge ili mafunzo yanayotolewa na Taasisi hiyo yawe na tija kwa waandishi wanaotoa taarifa za Bunge kwa wananchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi