Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba akisisitiza jambo wakati akifunga kikao kazi cha Bodi ya Ushauri ya NFRA jijini Dodoma hivi karibuni.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Serikali imeweka bayana mpango mkakati wa kuhakikisha kuwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) unajiendesha kibiashara pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba amebainisha mkakati huo jijini Dodoma wakati akifunga kikao kazi cha Bodi ya Ushauri ya NFRA hivi karibuni.
Mhe. Mgumba amesema kuwa serikali imetathmini mwenendo wa NFRA katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo na kujiridhisha kuwa umeanza kutekeleza majukumu yake ipasavyo hivyo kuongezewa jukumu muhimu la kununua nafaka kwa ajili ya kuhifadhi kadhalika kujiendesha kibiashara.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omary Mgumba akisisitiza jambo wakati akifunga kikao kazi cha Bodi ya Ushauri ya NFRA jijini Dodoma hivi karibuni. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Mhandisi Yustas Kongolle (Kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa NFRA Ndg Milton Lupa (Kulia).
Ameutaka wakala huo kufanya manunuzi ya mazao kwa ajili ya kuhifadhi kama akiba kwenye maghala ya serikali lakini pia kwa ajili ya biashara kwa kutafuta masoko ndani na nje ya Nchi.
Naibu Waziri Mgumba amesema wakala huo una jukumu la kuhifadhi mazao ya kila aina na siyo kuchagua mazao ya kuhifadhi akitolea mfano Mahindi kuwa ndiyo yamekua yakipewa kipaumbele ukilinganisha na mazao mengine.
Amesema kuwa serikali imetekeleza maelekezo ya ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya ujenzi wa maghala na vihenge vya kisasa hivyo NFRA inapaswa kuhakikisha kuwa inanunua nafaka ya kutosha kwa ajili ya kuhifadhi kadhalika kufanya biashara.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe Omary Mgumba akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) mara baada ya kuhitimisha kikao kazi hicho kilichofanyika Jijini Dodoma hivi karibuni.
Amesema kuwa NFRA inapaswa kununua mahindi, mpunga na mtama kwani Mazao hayo ni fursa kutokana na uhitaji mkubwa wa Chakula nchini na nje ya nchi.
"Unaweza kuwa na fedha nyingi lakini Kama huna mipango mizuri ya ununuzi huwezi kupata Mazao hivyo NFRA ni lazima mjipange vizuri ikiwemo kuongeza vituo vya ununuzi" Alisema na kuongeza kuwa
"Msije mkanunua mahindi kisiasa, ni lazima mtenganishe siasa na biashara, mkifanya hivyo mtajichimbia shimo wenyewe, hivyo lazima mkafanye biashara kwa ajili ya kupata faida"
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Mhandisi Yustas Kongolle akizungumza wakati wa kikao kazi cha Bodi ya Ushauri ya NFRA jijini Dodoma hivi karibuni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Yustas Kongolle ameishukuru Wizara ya Kilimo kwa kuwaamini yeye na wajumbe wa bodi hiyo kiasi cha kuwateua kuhudumu kwa miaka mitatu huku akisema watafanya kazi kwa bidii na weledi mkubwa zaidi.
"Kuaminiwa na Wizara maana yake Nchi imetuamini, tunaahidi kufanya kazi kwa bidii na kutimiza maagizo yote ambayo tumeelekezwa kufanya ikiwa ni pamoja na kuifanya NFRA ijiendeshe kibiashara," Amesema Mhandisi Kongolle
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) Delphina Mamiro ambaye ni Mjumbe wa Bodi hiyo ya NFRA amesema kuwa Bodi hiyo imejipanga kufanya kazi kubwa na nzuri zaidi ili kutekeleza imani hiyo.
Amesema kuwa mradi wa ujenzi wa maghala na Vihenge vya kisasa utakamilika hivi karibuni hivyo kuna jukumu kubwa na muhimu la kuhakikisha kuwa utekelezaji wa ununuzi unakamilika kwa wakati.