Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tumedhamiria, Tunachapakazi, Tunatekeleza
Jun 19, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_3754" align="aligncenter" width="706"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mabarawa wakipita katika katika ya mfano wa Reli ya kisasa ya kiwango cha Kimataifa itakayojengwa nchini.[/caption]

Na Dkt. Hassan Abbasi

NIANZE kwa kuwakaribisha wasomaji katika mfululizo wa makala hizi zitakazojikita katika kueleza mikakati ya Serikali, utekelezaji wake na changamoto katika kufikisha huduma muhimu kwa wananchi. Ni kwa minajili hiyo basi, safu hii itakuwa kiungo kati ya mwananchi na Serikali yake kwani watapata pia fursa ya kutoa maoni yao kwetu.

Katika makala hii na ijayo nitaanza kwa kueleza dira kuu ya nchi yetu na kuainisha mikakati muhimu ya kuifikia dira hiyo. Tutaainisha pia utekelezaji wa mikakati hiyo kabla ya kuwapa nafasi wasemaji wa kila wizara na baadaye taasisi za umma, mikoa halmashauri na wilaya nao kueleza utekelezaji katika ngazi zao.

Tanzania Tuitakayo

Mtu akiniuliza Tanzania inataka kwenda wapi, kwa maana ya dira, nitasema jibu la hili halihitaji mtu kutafuta vitabu au tafiti zilizofanywa. Jibu ni rahisi tu; tunataka Tanzania yenye neema tele. Ni bahati nzuri kwamba dira hii ya kila mmoja wetu kutaka nchi yetu ifikie kiwango hicho cha “neema tele” imetafsiriwa vyema na kuwekewa mwongozo.

Mwongozo huo si mwingine bali Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025. Katika Dira hiyo utakutana na azma ya nji yetu kutaka kuingia katika uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. Uchumi wa kipato cha kati ni sehemu tu ya safari ya kuendelea kuitafuta Tanzania yenye neema tele.

Dhana ya “Tanzania yenye neema” imefafanuliwa katika misingi mitano ya Dira ambayo ndiyo inapaswa kuwa malengo ya kufikiwa (key result area) katika kila mkakati tutakaouweka iwe ilani ya Chama tawala au Mipango ya muda mfupi ya maendeleo. Misingi hiyo ni:

Maisha bora

Katika nadharia ya maendeleo inayoungwa mkono na wasomi wa kisiasa wa aina ya Mwalimu Nyerere, maendeleo hutafsiriwa kuwa ni juhudi zote za kuyabadili na kuyaboresha maisha ya mwanadamu. Katika kufikia Tanzania yenye neema, Dira yetu inasisitiza Serikali kuweka mikakati ya kufikia azma hii.

Ukisoma andika la Dira utaona eneo hili linamhusu Mtanzania; maisha yake, shughuli zake, mahusiano yake na kila jambo linaloweza kufanyika kumsaidia Mtanzania kufikia maisha “yenye neema,” ikiwemo usawa katika kipato.

Dira inasema: “Kwa Tanzania dhana ya maendeleo ni kwamba kila kipato kinachopatikana basi kutawanyike kwa haki kwa kila mwananchi na usiwe na vikwazo vya kitaba au kijinsia katika kufaidi matunda hayo.”

Utawala Bora

Utawala bora ni msingi wa maendeleo kwa sababu pasipokuwa na misingi ya kisheria, utii wa sheria, utoaji wa haki kwa wananchi hata lengo la kwanza la dira kama tulivyoliona hapo juu halitafikiwa. Ndio maana Dira inasisitiza kuwa msingi wa utawala wa sheria uwekewe mikakati madhubuti.

Katika hili Dira inasisitiza: “Kufikia 2025 dhana ya utawala bora lazima iwe sehemu ya misingi ya maendeleo ya uchumi jamii ili kuleta uwajibikaji na kusaidia mapambano dhidi ya rushwa na maovu mengine katika jamii.”

Uchumi Imara

[caption id="attachment_3757" align="aligncenter" width="750"] Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John pombe Magufuli akibonyeza kitufe kuashiria kuzindua Mfumo wa Ukusanyaji Mapato kwa Njia ya kielektroniki akishuhudiwa na Makamu wa Rais Mhe Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine kwenye sherehe zilizofanyika Kijitonyama jijini Dar es salaam June 1, 2017.[/caption]

Hatuwezi kuzungumzia amani na utawala bora kama nyenzo za kuwaletea wananchi maendceleo bila kuwekwa misingi imara ya kukuza uchumi ili kuwapatia wananchi maendeleo. Uchumi imara huzaa Taifa imara na ndio msingi mkuu wa kuifikia “Tanzania yenye neema.”

Dira imeliona hili na inasisitiza: “Tanzania inapaswa kuwa na uchumi imara na unaotegemea sekta nyingi ambao unaweza kuhimili changamoto mbalimbali za kimaendeleo na kuhimili mabadiliko ya kijamii na kiteknolojia.”

Amani na Usalama

Unaweza kuwa na uchumi imara na ila kitu katika Taifa lakini kukosekana kwa usalama na amani kunaweza kuathiri yote tena ndani ya usiku mmoja. Tanzania imekuwa nchi ya amani ikilinganishwa na mataifa mengi Afria na duniani. Amani hii ni johari ya thamani.

Dira yetu imebaini hilo na imesisitiza kuwa amani na usalama wa raia na mali zao na Taifa kwa ujumla vinapaswa kujengwa, kuendelezwa na kulindwa kwa kiwango cha juu kabisa. Dira katika hili inasema:

“Ingawa Tanzania imekuwa na amani na umoja wa kitaifa, tunu hizi ni lazima ziendelee kuenziwa, kuimarishwa na kuendelezwa kama nguzo kuu za kufikia malengo ya Dira hii.”

Watu Walioelimika

Katika hili hakuna anayeweza kubishana kuwa elimu ni ufunguo wa maisha na ndio msingi mkuu wa mafanikio ya mwanadamu katika jitihada zake za kukabiliana na changamoto za kimaisha. Kwa kuona umuhimu huu wa Dira inasema kuwa na Taifa lenye watu walioelimika na kupata stadi muhimu za kiufundi ni muhimu sana.

Dira inasema: “Kuwa na watu wenye mawazo ya kimaendeleo ni muhimu lakini huwezi kuwa na watu hao bila elimu. Tanzania itajibariki yenyewe iwapo itahakikisha inakuwa na raia wenye ujuzi, ubunifu ili kuhimili ushindani.”

Katika eneo hili Dira inasisitiza Serikali kuweka mikakati ya kuwa na si tu raia walioelimika lakini pia wenye mtazamo chanya katika kuipenda nchi yao, kuchukia maovu, kufanyakazi kwa bidii, wanaojiamini na wenye kuheshimu mawazo ya wengine.

Katika kufikia azma hizi za Dira Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali na kupitia mifumo mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha maisha bora kwa kila Mtanzania. Miongoni mwa mikakati hiyo ni kutekeleza ilani ya chama tawala ambapo cha kwa sasa ni Chama cha Mapinduzi (CCM), kuweka mipango ya miaka mitano na kuanzisha mifumo ya utekelezaji kama BRN na kuunda taasisi mbalimbali kama Tume ya Mipango.

Wiki ijayo nitafanya tathmini ya jumla tu kuhusu namna miaka nane sasa kabla ya kufikia mwaka 2025 tunakwenda vipi katika kufikia malengo ya Dira na nitasisitiza mambo kadhaa kwa ajili ya faida ya umma.

Baada ya makala hiyo, kwa kuzingatia kuwa utekelezaji wa mikakati mbalimbali ya kufikia malengo haya ya Dira unahusisha ngazi zote kama vile Wizara, taasisi na mashirika ya umma na mikoa na halmashauri, basi makala zitakazofuata zitahusisha kusikiliza kutoka kwa watekelezaji wenyewe walioko katika maeneo yao.

Alamsiki.

*Mwandishi wa makala haya ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali. Anapatikana kwa baruapepe: mih@habari.go.tz.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi