Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Kujenga Mabwawa 14 na hekta 10,000 za Umwagiliaji kwa ajili ya Uzalishaji wa Mbegu
Jun 16, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Picha ya pamoja ya Wajumbe mbalimbali waliohudhuria Semina hiyo Walioketi. Katikati ni Waziri waKilimo Mhe. Hussein Bashe.

Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema kwa Mwaka wa fedha ujao Wizara yake itatumia Shilingi bilioni 420 katika ujenzi wa miundombinu ya Skimu za umwagiliaji ikiwemo Hekta elfu kumi kwa ajili ya uzalishaji wa Mbegu ambapo wadau wa sekta binafsi watapewa kipaumbele kwa ajili ya kuzalisha Mbegu na ujenzi wa mabwawa 14 yatakayokuwa na miundombinu ya umwagiliaji kwa matumizi ya kilimo na mifugo. 

 Aliyasema hayo leo mkoani Morogoro wakati akifungua semina ya siku mbili iliyowahusisha wadau wa Sekta ya Umwagiliaji mjini Morogoro ambapo Waziri Bashe ameendelea kusema kuwa utekelezaji wa kazi hiyo utakwenda sambamba na kuanzishwa kwa Ofisi za Umwagiliaji za Wilaya nchi nzima pamoja na kuajiri wasimamizi wa Skimu za umwagiliaji watakaohusika kusimamia zoezi la ukusanyaji wa ada na tozo za umwagiliaji kwa uhakika. 

Eneo lingine la kipaumbele kwa Waziri Bashe ni pamoja na kuwasaidia Wakulima Wadogowadogo kupata Teknolojia bora za kilimo cha umwagiliaji kwa bei nafuu ili waweze kupata tija na kuchangia ongezeko la mavuno katika sekta ya umwagiliaji, zoezi hilo litawahusu pia Vijana wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw, Raymond Mndolwa amewataka watumishi wote wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kufanya kazi kwa bidii na ubunifu ili kutimiza matarajio yaliyowekwa na Serikali, akiamini taasisi yake ina uwezo wa kutekeleza majukumu yaliyopangwa na Serikali kwa wakati, ufanisi na ubora unaotakiwa katika kuhudumia wananchi. 

“ Nitamsaidia kila mtumishi aweze kutimiza wajibu wake, tumejipanga na lililopo mbele yetu tunaweza kulitekeleza”, alisema Bashe.

Semina hiyo ya siku mbili imewashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi, Wakulima wadogo, Wataalam waBenki, Vyama vya Ushirika, Wahandisi na Maafisa kilimo wa Wilaya ikiangazia namna ya kuboresha maeneo matatu muhimu katika kilimo cha umwagiliaji, uzalishaji, huduma za umwagiliaji na njia bora yakukusanya Ada na Tozo za Umwagiliaji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi