Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

“Tume ya Haki za Binadamu Ina Jukumu Kubwa la Kulinda Haki za Wanawake na Watoto”-Balozi Seif
Jun 03, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_52976" align="aligncenter" width="750"] Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akifafanua jambo alipokutana na kufanya mazungumzo na ugeni wa Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora walipomtembelea ofisini kwake leo Juni 3, 2020 Vuga Mjini Zanzibar.[/caption]

Na. Paschal Dotto-MAELEZO.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi ameitaka Tume ya Haki za Binadamu Tanzania kufanya wajibu wake wa kuwaelimisha wananchi kuhusu haki ili kuelewa haki zao pindi wanapokuwa na matatizo mbalimbali ya kijamii kwa kufanya kazi kwa karibu na Serikali na kutekeleza majukumu yake kwa lengo la kuwatumikia vyema Wananchi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Akizungumza ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar alipotembelewa na ujumbe wa Tume hiyo wakiongozwa na Mwanyekiti wake, Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina, alisema Zanzibar imekuwa na matukio mengi ya unyanyasaji wa kijinsia jambo ambalo Tume hiyo inapaswa kuwaelimisha wananchi kuhusu upatikanaji wa haki pamoja na wakuwaeleza madhara ya unyanysaji wa kijinsia, kwani kufanya hivyo kutaisaidia Serikali Kuu kupata nguvu na uwezo wa ziada wa kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi hususan wanawake, watoto na hata wananchi wenye mahitaji maalum.

[caption id="attachment_52975" align="aligncenter" width="750"] Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akipokea kitabu kinachohusu masuala ya haki za binadamu na utawala bora kutoka kwa Mwenyekiti na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Mstaafu Mathew Mhina, walipomtembelea ofisini kwake leo Juni 3, 2020 Vuga Mjini Zanzibar.[/caption]

“Tume ya Haki za Binadamu ina kazi kubwa katika kutekeleza majukumu yake kwa upande wa Zanzibar kutokana na migogoro na changamoto nyingi zinazowakabili wananchi hali inayosababisha mitafaruku na mifarakano miongoni mwa jamii yenyewe, kwa hiyo nyie kama tume waelimisheni wananchi wa Zanzibar kufahamu sehemu ya kupata haki zao, lakini pia nyie mna jukumu kubwa la kusaidia kutatua migogoro na mifarakano inayotokea ya wananchi kusumbuliwa katika maeneo tofauti nchini Alisema Balozi Seif .

Aidha , Balozi Seif aliueleza uongozi wa Tume ya Haki za Binadamu kwamba yapo matatizo mengi yanayowakabili wananchi hasa wanawake ya kupewa ovyo talaka na matokeo yake kutelekezwa na waume zao sambamba na kuachiwa watoto bila ya huduma hali ambayo inakuwa ni kazi kwao kutimiza majukumu ya kulea watoto.

Alitahadharisha kwamba tabia hii iliyoanza kuota mizizi kwa baadhi ya wanaume wasiojali utu wa binadamu ni ya hatari kwa mtoto kwa vile inawakosesha haki zao za msingi kama vile kupata elimu na huduma za afya kwa sababu ya kutokuwa na ushirikiano wa kimalezi baina ya pande mbili.

[caption id="attachment_52974" align="aligncenter" width="750"] Makamu wa Pili wa Rais, Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi, akifanya mazungumzo na ugeni wa Mwenyekiti na Wajumbe wa Tume ya Haki za Binadamu, Walipomtembelea ofisini kwake leo Juni 3, 2020 Vuga Mjini Zanzibar, kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Msataafu, Mathew Mhina, Makamu Mwenyekiti, wa Tume ya Haki za Biadamu na Utawala Bora, Mohamedi Khamis Hamadi, Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu Zanzibar, Khatibu Mwinyi Chande na Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania Bara, Bi. Amina Talib Ali.[/caption]

Pia alieleza suala la udhalilishaji wa wanawake na watoto linaloikumba Dunia, hivyo watendaji na viongozi wa Tume ya Haki za Binadamu lazima wajikite zaidi kushirikiana na Taasisi za utoaji haki pamoja na wananchi katika vita ya kukabiliana na tatizo hilo linalochangia kupotoshwa kwa maadili ya jamii.

Kwa sasa masuala ya wanawake na watoto kudhalilishwa limekuwa ni jambo ambalo duniani kote ni mtihani, kwa hiyo Tume ya Haki za Binadamu jikiteni zaidi katika kufanya upembuzi wa suala hili, ili Taasisi za utoaji haki na Serikali ipate kuwasaidia wananchi kupitia nyinyi, lakini pia misisahau kutoa elimu kuhusu haki zao kwani hiyo pia itawasaidia kupambana na wahalifu na wavunjaji wa haki za Binadamu, alisema Balozi Seif.

Akijibu ombi la Tume ya Haki za Binaadamu la kupewa jengo la ofisi kwa upande wa Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliushauri ujumbe wa Tume kuwa na mpango wa kujenga majengo ya kudumu ya ofisi zake Visiwani Zanzibar kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kutoa maeneo ya ujenzi huo wakati wowote pale itapohitajika kutekelezwa mpango huo.

[caption id="attachment_52973" align="aligncenter" width="750"] Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (katikakati), akiwa kwenye picha ya pamoja na ugeni wa Wajumbe wa Tume ya Haki za Bianadamu na utawala bora wakati wa ziara ya tume hiyo katika ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar leo Juni 3, 2020,[/caption]

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania Jaji Mstaafu Mathew Pauwa Mhina, alisema Taasisi hiyo ni chombo cha umma kilichoundwa kusimamia upatikanaji wa Haki za Binadamu ili kusimamia Utawala Bora hapa nchini na kuwawezesha wananchi kupata haki zao za msingi pale inapohitajika .

“Tume ya haki za binadamu imeundwa na viongozi wake waliteuliwa na Mhe. Rais John Pombe Magufuli ili kutetea haki za Watanzania bila kujali imani zao, kwa hiyo utekelezaji wa majukumu yake upo kwa ajili ya wananchi wanaopokonywa haki zao, lakini pale ambapo watandaji wa Tume wakienda tofauti ni masuala ya kibinadamu ya kuteleza katika Utekelezaji wa majukumu yao, hivyo Viongozi Wakuu wanapaswa kushauri pale Watendaji hao wanapoteleza katika maeneo yao ya Kazi, Jaji Mstaafu Mathew Mhina.

Aidha Tume ya Haki za Binadamu Tanzania kupitia Mwenyekiti wake iliipongeza Serikali ya Jamahuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa inayoifanya ya kuhudumia wananchi jambo ambalo uongozi wa Tume hiyo unaliunga mkono.

Makamishina wa Tume ya Haki za Binadamu Tanzania waliteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli mnamo Tarehe 19 Septemba Mwaka 2019, ili kuhakikisha kunakuwepo na upatikanaji wa haki kwa watanzania katika maeneno yote ya Kijamii.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi