Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tume Kuweka Bei Elekezi ya Madini
Jul 31, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Jonas Kamaleki- MAELEZO, Dodoma

Serikali itapanga bei elekezi ya madini ili kuwawezesha wachimbaji wadogo na wakubwa kunufaika na kazi yao.

Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Tume ya Madini Nchini, Prof. Idris Kikula akiwa katika ziara ya ukaguzi wa shughuli za uchimbaji wa madini Mkoani Dodoma.

Imebainika kuwa wachimbaji wa madini ya jasi (Gypsum) wanalipwa fedha kidogo kwa tani moja kiasi kwamba gharama za uzalishaji ni kubwa kuliko bei wanayopewa.

Mchimbaji wa madini katika kijiji cha Manda, Wilaya ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma, Saimon Msanjila amesema kuwa gharama ya uchimbaji wa madini ya jasi tani moja na kuisafirisha hadi Dar es Salaam inafikia Shilingi 65,000 na bei anayopewa ni Shilingi 77,000.

“Kwa kweli bei tunayopewa na wawekezaji wa viwanda vya saruji ni ndogo sana, hivyo tunaiomba Serikali itusaidie katika hilo”, alisema Msanjila.

Katika ziara hiyo wanakijiji cha Manzase, Wilayani Chamwino walisimamisha msafara wa Tume ya Madini ili kueleze dukuduku lao kwa uwekezaji unaoendelea katika eneo lao.

Hoja zao zilikuwa ni kumtaka mwekezaji atimize ahadi yake ya kuwajengea daraja na kukarabati shule ya msingi.

Baada ya kuwasikiliza, Prof. Kikula alimtaka mwekezaji huyo kufika kwenye ofisi ya madini kesho yake kwa hatua zaidi.

Wanakijiji wa Manzase na Manda kwa pamoja waliishukuru Tume kwa kuwajali na kubaini changamoto walizonazo ili kuzipatia ufumbuzi.

Aidha, Prof. Kikula amemtaka mwekezaji  wa mawe ya nakishi kutangaza bidhaa zake kwani zinaonekana zina ubora na zinafaa kwa ujenzi, hasa katika Makao Makuu.

Rai hiyo ameitoa katika kijiji cha Mapanga, Kata ya Itiso, Wilayani Chamwino.

Kwa upande wake, Mwekezaji katika mgodi huo, Sisti Mganga amesema soko la ndani ni dogo hivyo akaonyesha umuhimu wa kupata masoko ya nje.

“Tunapanga kutafuta masoko nje na pia tutajenga kiwanda cha kutengeneza mapambo ili tusipoteze chochote tunachochimba, na tumepanga kuajiri watu wengi kwani kazi hii inahitaji nguvukazi kubwa”,alisema Mganga.

Sisti amesema anaunga mkono juhudi za Rais John Pombe Magufuli za ujenzi wa viwanda

Ziara hiyo ni endelevu kwani changamoto za wachimbaji hasa wadogo ni nyingi na pia Serikali inataka ikusanye maduhuli yake kupitia sekta ya madini.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi