Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TUGHE Yaipongeza WCF Kwa Kuwaandalia Mafunzo Kuhusu Fidia Kwa Wafanyakazi
Oct 03, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu, MOROGORO.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya TUGHE taifa, Bw. Hery Mkunda, ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kwa kuandaa mafunzo kwa ajili ya viongozi na watendaji wa chama hicho kuhusu Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi.

Bw. Mkunda aliyasema hayo Mjini Morogoro Oktoba 1, 2018  wakati wa semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo viongozi na watendaji wa TUGHE na kuwapa elimu kuhusu wajibu na haki za waajiri na wafanyakazi katika kutekeleza sheria hiyo.

Semina hiyo ya mafunzo ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano Mkuu wa kwanza  wa Wadau wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) uliofanyika mjini Arusha Mwaka jana (2017) ambapo pamoja na mambo mengine wadau walielekeza Mfuko kutoa mafunzo kwa makundi mbalimbali vikiwemo vyama vya wafanyakazi.

“Tuna wanachama takriban 70,000 kwa hiyo TUGHE sio jeshi dogo ni kubwa sana na hawa hapa ni watendaji wetu kutoka nchi nzima na ndio wanaohusika moja kwa moja na wanachama, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa WCF kwa kuandaa semina hii.” Alisema Katibu Mkuu huyo wa TUGHE Bw. Mkunda.

Alisema watendaji na viongozi wa TUGHE Tanzania nzima ambao wameshiriki mafunzo hayo, wakielewa vema majukumu ya Mfuko itawezesha viongozi hao kueneza elimu hiyo kwa wanachama wao.

“Kwa makatibu wetu wa mikoa ambao ndio wanaosimamia haki na maslahi ya wafanyakazi sehemu zao za kazi itakuwa ni rahisi sana kuhakikisha kwamba wafanyakazi ambao ni wanachama wetu wanapata haki zao ambazo Mfuko unatakiwa kutoa endapo wanapata madhara yatokanayo na kazi kama kuumia, kuugua au kufariki wakati wakitekeleza wajibu wao wa kazi” alisema Bw. Mkunda.

Akitoa neno la utangulizi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Mkurugenzi wa Uendeshaji Bw. Anselim Peter alisema, semina hiyo ya mafunzo ni muendelezo wa hatua ya Mfuko kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ambayo ni wadau wa Mfuko na nia kubwa ni kuwajengea uelewa wa madhumuni ya kuanzishwa kwa Mfuko, Sheria na jinsi Mfuko unavyofanya kazi. Alisema katika kipindi cha zaidi ya miaka miwili tangu Mfuko uanze kutekeleza majukumu yake, kumekuwepo na mafanikio makubwa ya kutimiza jukumu kuu la kuanzishwa kwa Mfuko la kupokea madai na kulipa fidia na hadi sasa Mfuko tayari umekwishalipa fidia zaidi ya shilingi bilioni 4.4.

Aidha Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi Sekta ya Hifadhi ya Jamii Nchini (SSRA) Dkt. Irene Isaka, aliwataka viongozi na watendaji wa Chama hicho kuhakikisha wanachama wao wanafahamu wajibu na haki zao katika Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF). Dkt. Isaka ameyasema hayo katika hotuba ya ufunguzi wa mafunzo ya Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi kwa viongozi na watendaji wa TUGHE taifa na mikoa   iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Utafiti na Tathmini SSRA, Joseph Mutashubilwa mjini Morogoro Jumatatu Oktoba 1, 2018.“ Kwa kufanya hivi tutakuwa tunaepusha migogoro na tunadumisha mahusiano mazuri sehemu za kazi hali itakayowavutia wawekezaji kuja nchini kwa wingi na hivyo kutimiza dhamira ya Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.” Alisema.

Dkt. Isaka pia amewataka washiriki hao wa mafunzo kusambaza elimu watakayoipata kwa kuwafikia na kuwapa elimu hiyo wanachama wa chama hicho na kumtaka kila kiongozi/ mtendaji aliyeshiriki awe na mpango kazi utakaoonesha idadi ya wanachama alionao katika eneo lake na namna atakavyowafikishia elimu hiyo ambayo ni muhimu kwao kuifahamu.“ Nina imani kwa kufanya hivi tutakuwa tumewasaidia kwa kiasi kikubwa wanachama wetu kuujua Mfuko, kazi zake na pia kufahamu nini wanapaswa kufanya baada ya kupata matatizo wakati wakiwa wanatekeleza majukumu ya mwajiri” alifafanua. Akinukuu kifungu cha 72 (4) cha Sheria ya Fidia kwa wafanyakazi, Mkurugenzi Mkuu huyo wa SSRA alisema kifungu hicho cha sheria kinatamka nafasi ya uwakilishi wa vyama katika kamati za afya na usalama mahali pa kazi ambapo mwajiri anatakiwa kutunza kumbukumbu hizo na kamati inatakiwa kukagua ili kuona kama hilo linafanyika. Hayo yote ni katika kuhakikisha kwamba upo ushirikishwaji baina ya viongozi/watendaji na Serikali katika kulinda afya za wafanyakazi sehemu za kazi.

[caption id="attachment_36214" align="aligncenter" width="750"] Watendaji na Viongozi wa TUGHE wakkifuatlia kwa makini mada inayohusu sheria ya fidia kwa wafanyaki katika mafunzo ya elimu juu ya Fidia kwa Wafanyakazi.[/caption]

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi