Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imetoa kiasi cha shilingi trilioni 1.2 katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji mkoa wa Dar es Salaam na Pwani mbapo upatikanaji wa maji umefikia asilimia 93.
Hayo yamebainishwa leo, Machi 11, 2025 jijini Dodoma na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), Mhandisi Mkama Bwire wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za Idara ya Habari- MAELEZO kuhusu mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita.
"Miradi iliyokamilika na inayoendelea ni mingi kwa sasa ambapo miradi ya maji safi imetengewa shilingi bilioni 800 huku miradi ya maji taka ambayo ni huduma ya usafi wa mazingira ni shilingi bilioni 400" amesema Mha. Bwire
Aidha, amefafanua kwamba, miradi ya shilingi bilioni 345 imekamilika hii ikiwa ni shilingi bilioni 330 kwa miradi ya maji safi na shilingi bilioni 15 kwa miradi ya maji taka na bado mingine inaendelea.
"Kutokana na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji ikiwemo mabwawa ya maji yaliyojengwa, yanayojengwa, yanayoboreshwa na yaliyoko kwenye mpango wa ujenzi Dar es Salaam, imefikia asilimia 93 ya utoaji huduma ya maji kwa wananchi.
"Ninaposema asilimia 93 nina maana kwamba, yapo maeneo yanapata maji kwa asilimia 100, 80, 70, au 60, kwa wastani wake tunapata hiyo asilimia tajwa, na kufikia mwishoni mwa mwaka huu 2025 tutatimiza lengo la Ilani ya CCM ya kufikia asilimia 95 kwa maeneo ya mijini" - Mha. Bwire.
Ametaja miradi hiyo ambayo imeleta mafaniko ya upatikanaji wa maji kwa asilimia 93 kuwa ni pamoja na mradi wa Chalinze awamu ya tatu, mradi wa maji Chuo Kikuu hadi Bagamoyo, mradi wa maji Mshikamano, mradi wa maji Kimbiji - Kigamboni, na mradi wa maji Dar es Salaam Kusini huku miradi mingine ikiendelea na mingine ikiwa kwenye mpango wa kuanza.