Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Treni ya SGR Kuanza Kazi Disemba
Jul 09, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Dkt. Leonard Chamuriho amesema treni ya umeme itakayotumia reli ya kisasa SGR kutoka Dar es salaam hadi Morogoro itaanza kazi disemba mwaka huu.

Akizindua Bodi mpya ya Wakurugenzi wa Shirika la Reli nchini (TRC) Jijini Dar es salaam leo Waziri Chamuriho ameitaka Bodi hiyo kwa kushirikiana na Menejimenti ya TRC kuhakikisha maandalizi yote ya msingi ya kuwezesha kuanza kwa usafiri huo yanakamilika ifikapo mwezi Novemba.

“Hakikisheni treni ya kisasa itakayotumia reli ya SGR sehemu ya Dar es salaam hadi Morogoro inaanza ili kuwawezesha wananchi kunufaika na fursa hiyo mpya kiuchumi”, amesema Waziri Dkt. Chamuriho.

Waziri Dkt. Chamuriho amesema Serikali itaendelea kuikarabati reli ya sasa meter gauge na kuongeza vichwa vipya vya treni na mabehewa ili iendelee kutoa huduma katika ubora unaotakiwa wakati ujenzi wa reli ya kisasa SGR ukiendelea.

“ TRC ni lazima muwe na  maarifa ya kibiashara ili hatua ya Serikali kukarabati na kununua mabehewa mapya iendane na kasi ya kusafirisha shehena nyingi na mizigo mizito kwa reli na hivyo kupunguza mzigo mzito katika barabara”, amesisitiza Waziri huyo.

Amezungumzia umuhimu wa Bodi na Menejimenti ya TRC kuhakikisha maboresho ya muundo yanaendana na maslahi ya wafanyakazi ili kuongeza morali na kuleta tija katika shirika hilo.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya TRC, Prof. John Kondoro amesema wamejipanga kuhakikisha shirika linatoa huduma ya kisasa, haraka na kwa gharama nafuu na watahakikisha reli ya sasa inapitika wakati wote wa mwaka.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa TRC, Bw, Masanja Kadogosa amesema hadi sasa tayari asilimia 92 ya ujenzi wa reli ya SGR kati ya Dar es salaam na Morogoro umekamilika wakati sehemu ya Morogoro hadi Makotopora Singida ujenzi wake umefikia asilimia 65.

Kukamilika kwa reli ya SGR na uboreshaji unaofanywa katika reli yote ya sasa meter gauge kutahuisha huduma za usafiri na uchukuzi nchini na hivyo kuchochea uzalishaji na biashara za ndani na nje ya nchi na hivyo kukuza uchumi.

Katika hatua nyingine Waziri Dkt. chamuriho amezindua Bodi ya Chuo cha bahari DMI na kuitaka Bodi hiyo kuhakikisha inakisaidia Chuo hicho kuongeza idadi ya wataalam wa bahari, kuwa na takwimu sahihi za mabaharia hapa nchini na kuisaidia nchi katika adhma ya kufufua uchumi wa bluu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi