Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TRA Yakusanya Trilioni 3.8 Robo ya Kwanza ya Mwaka wa Fedha 2018/19
Oct 08, 2018
Na Msemaji Mkuu

 Na Veronica Kazimoto

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefanikiwa kukusanya jumla ya Shilingi Trilioni 3.84 kwa kipindi cha miezi mitatu ya Mwaka wa Fedha 2018/19 ikiwa ni kuanzia Julai hadi Septemba, 2018 ikilinganishwa na shilingi trilioni 3.65 ambazo zilikusanywa kipindi kama hicho katika Mwaka wa Fedha wa 2017/18.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi Richard Kayombo amesema kiasi hiki ni sawa na ukuaji wa asilimia 5.32 na kuongeza kuwa ukusanyaji wa mapato hayo umekuwa ukiongezeka kila mwezi.

“Katika mwezi Julai, 2018, TRA ilikusanya jumla ya shillingi trillioni 1.20 sawa na ukuaji wa asilimia 9.20, mwezi Agosti, 2018 jumla ya shilingi trillioni 1.27 zilikusanywa ikiwa ni sawa na ukuaji wa asilimia 5.86 wakati mwezi Septemba, 2018 mamlaka ilikusanya jumla ya shilingi trillioni 1.36 ambayo ni sawa na ukuaji wa asilimia 1.65,” alisema Kayombo.

Kayombo amewashukuru walipakodi wanaoendelea kulipa kodi zao kwa hiari na wakati na amewahimiza wale wote ambao bado wanasuasua kujitokeza kulipa kodi hizo na wale wenye changamoto mbalimbali wametakiwa kufika katika ofisi za TRA mikoani na wilayani ili kuonana na mameneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania.

Aidha, Kayombo amesema TRA inaendelea na zoezi la kupokea maombi ya misamaha ya riba na adhabu katika malimbikizo ya madeni ya kodi za nyuma ambapo ameeleza kuwa mpaka sasa jumla ya walipakodi 1,950 wamewasilisha maombi ya kusamehewa riba na adhabu ambayo yanafikia jumla ya shilingi bilioni 185.4.

Mwitikio wa walipakodi kuomba msamaha wa wa riba na adhabu ni mkubwa na unaridhisha na kuna baadhi ya walipakodi waliowasilisha maombi ambao wameshapewa majibu na wengine wako katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa maombi yao. Hivyo, nachukua fursa hii kuwakumbusha wafanyabiashara ambao hawajawasilisha maombi wawahi kuwasilisha maombi hayo kabla ya tarehe 30 Novemba, 2018.

Mkurugenzi Richard Kayombo ametoa wito kwa walipakodi na wananchi wote kwa ujumla kuendelea kulipa kodi kwa hiari na wakati na kuwaasa wale wote wanaojishughulisha na vitendo vya kugushi risiti za kielektroniki za EFD nchi nzima hasa maeneo ya Kariakoo, kuacha mara moja kwa sababu wakibainika watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi