NA OSCAR ASSENGA, TANGA
Meneja wa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA} Mkoa wa Tanga, Specioza Owure amesema mamlaka hiyo imevuka lengo la ukusanyaji wa mapato kwa zaidi ya asilimia 29.7 kwa mwaka 2020/2021.
Owure aliyasema hayo wakati akitoa taarifa ya mapato kwa mwaka 2020/2021 na mipango mikakati ya ukusanyaji mapato waliojiwekea mwaka 2021/2022.
Alisema mamlaka hiyo mkoani Tanga imefanikiwa kukusanya zaidi ya Sh.Bilioni 154.5 wakati lengo lilikuwa ni kukusanya Sh.Bilioni 140.2 ambao ni utendaji wa asilimia 110 katika ya makusanyo hayo.
“Idara ya kodi za ndani imekusanya zaidi ya Shilingi Bilioni 70.5 na Idara ya Forodha imefanikiwa kukusanya shilingi Bilioni 83.99 kwa mwaka 2020/2021“, alisema Meneja Owure
“Lakini kumekuwa na ongezeko la makusanyo kwa zaidi ya Bilioni 35.3 sawa na asilimia 29.7 ukilinganisha na makusanyo ya kipindi kama hicho kwa mwaka 2019/20 ambapo mkoa ulikusanya Sh Bilioni 3.99 sawa na asilimia 2.85", alisema Meneja Owure.
Alizitaja sababu ambazo ziliwawezesha kufikia hatua hiyo ya kuvuka lengo kwa mwaka huo ni kuendelea kuwa na uhusiano mzuri kati yao na viongozi wa mkoa na wilaya zote pamoja na taasisi zote za Serikali na walipa kodi.
Meneja huyo alisema pia lengo la TRA Mkoa wa Tanga kwa mwaka 2021/2022 ni kukusanya zaidi ya Bilioni 180.88.
Hata hivyo alisema pia wana mikakati ya kuvuka lengo kwa mwaka huu, TRA imejipanga kufanya usajili wa wafanyabiashara wapya ambao hawamo kwenye wigo wa kodi.
“Pia tuna mkakati wa kuendelea kufuatilia na kudai madeni ya kodi kwa ukaribu na kwa mujibu wa sheria", aliongeza Owure.
Meneja huyo alisema pia wataendelea kufanya doria kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama mkoa ili kuweza kubaini na kuzuia biashara za magendo.