Timu ya Makatibu Wakuu wa kisekta wametembelea na kukagua zoezi la ugawaji wa misaada ya kibinadamu ikiwemo vyakula kwa waathirika wa maafa yaliyosababishwa na maporomoko ya mawe na tope kutoka mlima Hanang.
Timu hiyo pia imekagua maeneo yaliyopata athari, na zoezi la kurejesha hali ya kawaida ikiwemo miundombinu ya Barabara na zoezi la kuondoa tope katika maeneo yaliyoathiriwa na maafa.
Ziara hiyo iliongozwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Dkt. Jim Yonazi tarehe 20 Desemba, 2023 ambapo amesema kuwa Serikali imeendelea na zoezi la kurejesha hali pamoja na ugawaji wa vyakula kwa waathirika wote wa maafa hayo huku hali ya kurejesha miundombinu ya barabara na kusafisha maeneo yaliyopata athari ikiendelea.
Akizungumza kuhusu zoezi la ugawaji wa vyakula kwa waathirika hao ameeleza kuwa, Serikali itahakikisha kila aliyepaswa kupata msaada anapata kwa wakati na kwa mgawanyo sawa na miongozo iliyopo na kueleza kuwa hakuna mtu atakayekosa chakula katika mgao huo.
“Serikali imeendelea na hatua za kurejesha hali kwa wakazi wa Hanang’, na hapa ujenzi wa mitaro unaendelea na utoaji wa tope zilizobaki, zoezi linaendelea vizuri na hadi sasa ni nyumba chache zimesalia kuondolewa tope,” ameeleza Dkt. Yonazi.
Aidha ametoa wito kwa wananchi waendelee kuwa na utulivu kwa kuzingatia namna Serikali inavyoendelea kuratibu ili kuhakikisha wanapata misaada kama iliyokusudiwa.
“Hadi sasa watu zaidi ya 186 ndiyo waliobakia katika zoezi hilo kati ya watu 1491 ambao walitakiwa kupata chakula, hivyo wote watapata chakula hakuna atakayekosa chakula, wapo waliopata awamu ya kwanza na sasa wanapewa awamu ya pili, na zoezi la kuhamisha watu kwenye makambi linaendelea na Serikali itahakikisha watu wanarejea katika hali zao,” amesisitiza.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa Gendabi waliopatiwa misaada ya vyakula, Bi. Stella Lili ameishukuru Serikali namna ilivyoratibu zoezi la ugawaji wa vyakula na kusema hatua hiyo imewapa faraja na kuonesha namna viongozi wanavyowajali.
“Tunashukuru tumepewa vyakula ikiwemo mahindi, mchele, unga wa sembe, unga wa ngano, mafuta, chumvi, maji ya kunywa pamoja na mahitaji mengine muhimu, hakika kwa hatua hii ninaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyoshughulikia maafa haya,” ameeleza Stella.