Wajumbe wa Timu Kuu ya Wataalamu ya Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 wapewa mafunzo kuhusu uandaaji wa Dira 2050 pamoja na nyenzo za utendaji kazi wa uandaaji wa Dira hiyo.
Akizungumza leo Januari 13, 2024 Zanzibar Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Bw. Lawrence Mafuru amesema kuwa lengo la mafunzo hayo ya Timu Kuu ya Wataalamu ya Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ni kujenga uelewa wa pamoja kwa Timu ya Wataalam ya Uandishi wa Dira kuhusu mchakato wa maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Tunafanya hivi ili kila mmoja wetu aelewe majukumu atakayo kuwa nayo katika uandaaji wa Dira na kufahamu hatua zote muhimu katika uandishi wa Dira, 2050. Vile vile kwa kuwa baadhi ya wajumbe katika timu hizi kitaaluma sio wanamipango na katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku hawajihusishi na shughuli za mipango ya maendeleo ni vyema tukapata fursa ya kukakaa pamoja na kubadilishana mawazo kabla ya kuanza rasmi kutekeleza majukumu yaliyo mbele yetu”, ameeleza Bw. Mafuru.
Naye, Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango Zanzibar, Dkt. Rahma Salim Mahfoudh amesema “Katika kuandaa Dira hii, ni vyema kuhakikisha kwamba tunakuwa na ushirikishwaji wa kutosha, tuangalie ule ushiriki ambao ulishafanyika na kuboresha zaidi. Tuweke Dira ambayo itakuwa na uhalisia”.
Vilevile, Mwenyekiti wa Timu Kuu ya Wataalamu ya Maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Prof. Lucian Msambichaka ameishukuru Serikali kwa kuwa na imani na Timu hiyo na kuipa jukumu hilo muhimu kwa taifa. Aidha, ameahidi kuwa Timu hiyo itafanyakazi kwa juhudi zaidi kwa kuwa Watanzania na dunia kwa jumla ina matarajio makubwa katika kuandaa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
“Ombi letu ni kupata ushirikiano katika ngazi mbalimbali za uongozi na makundi mbalimbali ya jamii. Pia Watanzania watoe ushirikiano ili tuweze kumaliza jukumu hili kwa muda uliopangwa na sisi tutafanyakazi nzuri kwa manufaa ya taifa”, amesema Prof. Msambichaka.