Na Judith Mhina – Maelezo
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) waunganisha Tanzania kwa kuongeza huduma ya minara ya mitandao Bara na Zanzibar kwa kujenga minara 181 passive part ambapo imekamilika, minara hiyo inakadiriwa kuwashwa kabla ya mwezi Oktoba 2022.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye ameyasema hayo leo wakati wa kuwasilisha Hotuba ya Bajeti ya Wizara yake leo Bungeni.
Akiwasilisha Hotuba hiyo, Waziri Nape amesema “ Serikali imeweza kuingia makubaliano na watoa huduma 161 wa Bara na visiwani, na minara hii itajengwa mipakani maeneo ya ofisi za Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zilikuwa hazina huduma za Mawasiliano”
Aidha, ameongeza kuwa kwa upande wa Zanzibar ujenzi wa minara 42 ipo katika hatua za ukamilishwaji ambapo ujenzi wa minara hiyo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2022. Pia minara mingine 119 ipo katika hatua za awali ikiwa ni pamoja na kutafuta maeneo kwa ajili ya ujenzi pamoja na kutafuta wakandarasi.
Mfuko wa Mawasiliano kwa wote una jukumu kubwa la kuhakikisha upatikanaji wa mawasiliano katika maeneo ya vijijini na maeneo ya mjini yenye mawasiiano hafifu maeneo yaliyo pembezoni mwa nchi na yasiyovutia uwekezaji kibiashara hayaachwi nyuma kwa kukosa mawasiliano.
Kwa kutambua hilo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa busara ikaanzisha UCSAF kuwezesha sekta binafsi katika kutoa huduma za mawasiliano kwa wote katika maeneo ya vijijini kimtandao, na kuwezesha Watanzania wote washiriki katika kukuza uchumi na maendeleo yao kwa kutumia teknolojia iliyopo.