Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TCU Yafuta Udahili Kwa Vyuo 19
Jul 25, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Paschal Dotto

Tume ya Vyuo vikuu (TCU) imevifutia udahili vyuo 19 na kufuta kozi 75 katika vyuo  22 kwa kukiuka Sheria taratibu na kanuni za utoaji wa elimu ya juu hapa nchini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii Jijini Dar es Salaam Jana Afisa habari wa Tume hiyo Bw. Edward Mkaku amesema uamuzi wa kuvifutia udahili baadhi ya vyuo ni kutekeleza agizo la serikali lililoitaka Tume hiyo kuvisimamia kwa karibu vyuo ili viweze kutoa elimu bora.

Bw. Makaku amesema kuwa kwa vyuo ambavyo wanafunzi wanaendelea na masomo mabadiliko haya hayatawahusu wanatakiwa kuendelea na masomo kama kawaida, ila vyuo hivyo  haiviruhusiwi kudahili wanafunzi wapya kwa mwaka huu wa masomo.

Alizitaja baadhi ya sababu zilizopelekea baadhi ya vyuo kufutiwa udahili wa Shahada, Shahada za Uzamili pamoja na Shahada za Uzamivu kuwa ni kukosa vitendeakazi na wataalam katika kufundisha elimu ya juu.

Aidha Mkaku amesema kuwa TCU imeandaa maonesho yatakayoanza Julai 26, 2017 katika viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam,maalum kwaajili ya kutoa elimu kwa wanafunzi wanaohitaji kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini, pia kuelezea shughuli mbalimbali zinazofanywa na Tume hiyo.

Bw. Mkaku pia amesema baadhi ya vyuo vinavyotoa taaluma za afya kama Kilimanjaro Chritian Medical College (KCMC) cha Mkoani Kilimanjaro, Kampala International University (KIU) cha  Jijini Dar es Salaam pamoja na  Hubert Kairuki Memorial University (HKMU) pia cha Jijini  Dar es Salaam ambavyo vilikuwa vikitoa kozi za udaktari, ufamasia pamoja na shahada ya uzamili katika Udaktari wa magonjwa ya kinamama iliyokuwa ikitolewa na Chuo cha Hubert Kairuki  imebainika kuwa hawakuwa na vifaa na wataalam wa kutosha kufundisha kozi hizo.

Alivitaja vyuo  vilivyofungiwa kutokana na kutokuwa na wataalam wa kutosha kuendesha kozi zake kuwa ni, St. Joseph, St. John, Tumaini University pamoja na vyuo vingine kadhaa ambavyo havina waalimu pamoja na vifaa kwa mujibu wa maelekezo ya Tume hiyo.

Bw.Mkaku amebainisha kuwa katika vyuo 22 hapa nchni kuna zaidi ya kozi 75 ambazo hazitakiwi kudahili wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2017/2018 na kuwashauri watahiniwa wanaotarajia kujiunga na mwaka huu wa masomo kuingia katika tovuti rasmi za vyuo  ili kujua kozi ambazo zinatakiwa na kozi ambazo zimezuiliwa.

“Tulifanya uhakiki wa vyuo hapa nchni Septemba na oktoba 2016 na kubaini baadhi ya vyuo kutokukidhi mahitaji ya watahiniwa katika baadhi ya kozi kwa hiyo ni muhimu kutoa taarifa mapema kwa umma juu ya  mchakato huu” Alisema.

Katika kuondoa changamoto kwa watahiniwa wa miaka ijayo Mkaku amesema kuwa maonesho ya vyuo yatakuwa yanafanyika kikanda ili kutoa elimu kwa umma katika masuala mazima ya elimu ya juu.TCU ilikabidhi rasmi jukumu la udahili kwa vyuo husika Julai 20,2017 ili waendeshe wenyewe na wao watabaki kuwa wasimamizi wa Sheria na sera za vyuo vya elimu ya juu.

TCU wametoa onyo kwa vyuo vitakavyoendelea kudahili wanafunzi katika kozi zilizofutwa kuwa ni kinyume cha Sheria na wakibainika watashitakiwa kwa mujibu wa Sheria za nchi na zile za vyuo vikuu.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi