Na Eliud Rwechungura
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza bidhaa zisizokidhi ubora wa viwango zenye thamani ya shilingi milioni 40 ambazo ziliondolewa sokoni na Wakaguzi wa TBS kanda ya kati kuanzia mwezi Novemba, 2020 hadi Januari 15, 2021.
Zoezi hilo la uteketezaji bidhaa hizo limefanyika katika dampo Chidachi - Dodoma, leo Januari 27, 2021
Bidhaa zilizoharibiwa ni pamoja na vipodozi vyenye viambata sumu, vyakula na vinywaji ambavyo muda wake wa matumizi umepita (Expired produducts) vilivyopatikana katika maduka mbalimbali yaliyopo katika Mikoa ya Dodoma, Tabora na Singida.
Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009 pamoja na Sheria ya Fedha Na.8 ya mwaka 2019 mbali na majukumu mengine zimelipa mamlaka Shirika kuondoa bidhaa hafifu sokoni na kuziharibu ama kuzirudisha zinakotoka pindi zinapobainika kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Wakaguzi wa TBS hufanya ukaguzi wa bidhaa viwandani na sokoni ili kujiridhisha na hali halisi ya soko na inapobainika uwepo wa bidhaa hafifu huondolewa sokoni na aliyekutwa na bidhaa hizo hulazimika kulipia gharama ya uteketezaji.
Mkaguzi wa udhibiti ubora TBS, Lazaro Msasaranga ametoa rai kwa wafanyabiashara wote kuhakikisha kuwa wakati wote wanazingatia masuala ya ubora kwa kuuza bidhaa za vipodozi na vyakula vilivyosajiriwa pamoja na ukomo wa matumizi wa bidhaa hizo ili kumlinda mlaji na kuepuka hasara ya kuharibiwa bidhaa hizo.
Aidha, wafanyabiashara wote wanatakiwa kusajili bidhaa za vyakula, vipodozi, majengo ya kufanyia biashara na maghara ya kuhifadhia bidhaa hizo.