Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TBS Yang’ara Kimataifa
Mar 18, 2025
TBS Yang’ara Kimataifa
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 18, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Na Frank Mvungi, Dodoma

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) imekuwa taasisi ya kwanza katika Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kupata ithibati (accreditation) ya mifumo ya udhibiti ubora wa bidhaa (Product Certification) ya kimataifa katika wigo mpana (wide scope) ndani ya muda mfupi na ni ya taasisi ya tatu kupata ithibati hiyo iliyotolewa na SADCAS Septemba, 2024 hivyo kufanya mifumo hiyo kutambulika kimataifa.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Dkt. Ashura  Katunzi wakati wa mkutano wake na Waandishi wa Habari leo Machi 18, 2025 jijini Dodoma uliolenga kueleza utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miaka minne.

”Pia kwa mwaka 2025, TBS imefanikiwa kupata ithibati ya umahiri wa mfumo wa usimamizi wa chakula katika kiwango cha kimataifa toleo jipya (ISO 22003:2022).” Alisisitiza Dkt. Katunzi.

Akieleza zaidi, Dkt. Katunzi amesema kuhamia kwenye ithibati hii kunaifanya TBS kuwa taasisi ya kwanza katika Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kupiga hatua hiyo.

Aliongeza kuwa ithibati hiyo ni ishara kuwa TBS inafanya kazi zake kwa kuzingatia miongozo ya kimataifa iliyowekwa na hivyo kuendelea kuaminiwa na wateja na wadau wengine.

Amesema TBS inajivunia kuwa na wataalamu wenye umahiri na weledi mpaka kutambulika kimataifa, kwani wataalamu wa TBS hualikwa na SADCAS kwa ajili ya kutoa msaada wa kitaalam katika masuala ya ithibati (accreditation) kwenye maeneo ya Metrolojia (metrology), uthibitishaji wa ubora (certification), na ukaguzi (inspection) kwa taasisi na mashirika yanayohitaji huduma hizo katika Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Sanjari na hiyo Dkt. Katunzi amesema, shirika kupitia wataalamu wake liliweza kutoa Mshindi wa ISO Next Generation Award kwa mwaka 2023, tuzo iliyoandaliwa na Shirika la Viwango la Kimataifa (ISO) ambayo ilikuwa na lengo la  kutambua mchango wa wataalam katika  kuandaa viwango vinavyochagiza maendeleo endelevu ya kimataifa (UN SDGs).

Shindano hilo lilihusisha maafisa viwango wenye umri chini ya miaka 35 kutoka nchi takribani 175 wanachama wa ISO na  mtaalam kutoka TBS aliibuka mshindi na  kukabidhiwa tuzo husika huko Brisbane, Australia.

TBS inaendelea na juhudi za kuweka na kutekeleza mikakati mbalimbali ili kuboresha huduma zake kwa lengo la kuwezesha biashara kwa madhumuni ya kuinua uchumi wa viwanda kwa kuchagiza uzalishaji wa bidhaa salama na bora hapa nchini kama njia mojawapo ya kuchangia pato la Taifa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi