Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

TBS Yajenga Maabara Dodoma, Mwanza
Mar 18, 2025
TBS Yajenga Maabara Dodoma, Mwanza
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita leo Machi 18, 2025, katika Ofisi za Idara ya Habari - MAELEZO, jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Dkt. Ashura Katunzi amesema katika kutekeleza azma ya Serikali kuhakikisha wananchi wanapata huduma kwa ukaribu na kupunguza gharama, shirika hilo limeanza ujenzi wa maabara katika mikoa ya kimkakati ya Dodoma na Mwanza.

Dkt. Katunzi amesema hayo leo Machi 18, 2025 katika ofisi za Idara ya Habari-MAELEZO jijini Dodoma wakati wa Mkutano na Waandishi wa Habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa shirika hilo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.

“Kwa upande wa Dodoma, maabara zitakazojengwa zitahudumia mikoa mitatu ya Kanda ya Kati ambayo ni Dodoma, Singida na Tabora pamoja na mikoa mingine ya karibu,” amefafanua Dkt. Katunzi.

Ameendelea kusema kuwa, maabara za Mwanza zinatarajiwa kuhudumia mikoa sita, ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu. Pia Shirika limeshapata Mshauri Mwelekezi (Consultant) wa kuchora michoro ya jengo pamoja na kusimamia ujenzi wa maabara na ofisi jijini Arusha.

Aidha, hatua hiyo ya ujenzi wa maabara itasaidia kusogeza huduma karibu na wananchi na kuongeza ufanisi katika utoaji wa majibu ya vipimo vya sampuli.

“Shirika limetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.7 kwa ajili ya kuimarisha ofisi saba za kanda (Arusha, Mwanza, Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma, Kigoma na Mbeya) pamoja na ofisi za mipakani (Tunduma, Kasumulo, Horohoro, Holili, Tarakea na Namanga),” amesema Dkt. Katunzi.

Ametaja ofisi nyingine zitakazoimarishwa kupitia fedha hizo kuwa ni Bandari ya Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Mwanza, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, Sirari, Kabanga, Rusumo, Mutukula, Bandari ya Bagamoyo, bandari ya Mbweni, bandari ya Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Kambarage Nyerere – Dar es Salaam pamoja na Bandari ya Tanga.

Ofisi hizo zitaimarishwa kwa kuongeza wafanyakazi na vitendea kazi kwa ajili ya kutoa huduma kwa wakati na kuimarisha zoezi la ukaguzi wa mara kwa mara sokoni ili kupunguza bidhaa hafifu sokoni na hatimaye kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora na salama.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi